Udanganyifu
Udanganyifu ni kitendo cha makusudi cha kusema uongo, kupotosha, au kuficha ukweli ili kumfanya mtu mwingine aamini jambo lisilo la kweli, mara nyingi kwa faida binafsi, kujilinda au kusababisha madhara. Ni kitendo kinachokiuka, kinachohusisha hila, ushawishi wa taarifa za uongo.
Kusudi: Hufanywa kwa makusudi ili kufanikisha lengo fulani kama kupata pesa au kumdhuru mtu kwa kumpoteza. Udanganyifu hufanyika kwa njia za injili za uongo ili Mkristo apotee kwenye ramani ya mbinguni.
Aina: Inaweza kuwa ya maneno ya uongo, vitendo (kuficha taarifa) au kupotosha.
Shetani ni baba wa uongo hulipinga Neno la MUNGU sana, kwa sababu Neno la MUNGU ni kweli; maana yeye yupo kinyume cha kweli.
Kwa ufupi udanganyifu ni hila yeyote inayolenga kupotosha ukweli kwa namna hizi mbili:
Shetani ameweka uongo kwenye imani; baadhi ya imani ni uongo, hakuna ukweli ndani yake. Kuna baadhi ya vitu shetani husema ukweli lakini wenye uongo ndani yake, lakini kuna wakati mwingine husema uongo wote. Kusudi la shetani bado ni lilelile, kumeza watu wengi na juhudi yake ni wote waende kuzimu.
[2]Ulimi wako watunga madhara, Kama wembe mkali, Ewe mwenye hila.
[3]Umependa mabaya kuliko mema, Na uongo kuliko kusema kweli.
[4]Umependa maneno yote ya kupoteza watu, Ewe ulimi wenye hila.
Shetani anajua kabisa kwamba MUNGU hachangamani na uovu, anataka ukweli mtupu katika kanisa; kanisa haliwezi kuwa na uongo ndani yake na MUNGU akawepo, ataondoka tu. MUNGU anataka tujue na kuishika kweli yote.
[7]Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli?
[8]Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi.
[9]Chachu kidogo huchachua donge zima.
Wateule ni watu maalum, waliotengwa kwaajili ya kwenda mbinguni. Yaani ni kwamba watu wengi wanaookoka baada ya kumuamini YESU, lakini wanaokidhi vigezo vya utakatifu ambavyo MUNGU ameweka ni wachache sana; hao ndio huitwa wateule. Maana halisi ya mteule ni mtu aliyeteuliwa, yaani anachaguliwa ndani ya waliochaguliwa kufaa kuliko wale wote.
[14]Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.
Ni uchambuzi; yaani unachambua kitu mara moja, mara mbili, mara tatu hata mara kadhaa mpaka pale umepata kiwango kizuri halisi unachotaka, kusiwepo na uchafu wowote juu ya hicho kitu. Hivi ndivyo MUNGU anavyofanya juu ya watu wote waliookoka; wateule ni watu ambao wamefikia kiwango anachotaka MUNGU. Shetani anawatafuta sana watu hawa; MUNGU anavyowaandaa, yeye anatafuta kuwapoteza.
[12]Kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;
[13]Hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.
Wakristo ni wengi sana; kila aliyeitwa kwenye neema ya MUNGU kwa njia ya YESU KRISTO, huyo ni Mkristo. Kila Mkristo ni mfuasi wa YESU KRISTO; mtu huyu ameamua kumfuata YESU.
[1]Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa MUNGU, naye Neno alikuwa MUNGU.
[2]Huyo mwanzo alikuwako kwa MUNGU.
[3]Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.
Kila kitu chema kinachofanyika hapa duniani kimebebwa na nguvu ya Neno la MUNGU; ndiyo maana shetani anafanya kila mbinu kulipiga vita Neno la MUNGU. Hakuna kilichofanyika pasipo kwa nguvu za MUNGU katika Neno lake. Biblia nyingi siku hizi hazipo salama; shetani ameharibu maana kamili ya mambo ndani ya Biblia, na amenyofoa jumbe kadhaa zenye kuokoa watu wasiishi katika kweli.
Mmiliki halisi aliyepewa hati miliki ya Biblia (Papa, kiongozi wa Katoliki) ndiye aliyepewa mamlaka na ulimwengu kwa nyakati hizi za mwisho, amehariri na kuondoa vitu muhimu ndani ya Biblia. Anasema yamepitwa na wakati, sheria ni ngumu hazipaswi kufuatwa. Leo hii nakushauri ununue Biblia na uitunze; kuna wakati ambao itakuwa ni vigumu sana kupata Biblia halisi yenye maana kamili MUNGU anayotaka.
[3]Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana.
[4]Lakini wema wake Mwokozi wetu MUNGU, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa.
Neno la MUNGU ni kweli; asiye na Neno la MUNGU na hamuamini YESU KRISTO, mtu huyo hana akili. Maisha ya kale yaani zamani tulikuwa hatuna akili kwa yale tuliyoyatenda; maana tulifanya ujinga na kuishi kama wajinga kwa sababu hatukuwa na Neno la MUNGU. Lakini sasa tuna akili maana BWANA YESU ametuokoa na kutupa akili.
Basi, zamani zile za ujinga MUNGU alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu.
Shetani anajua umuhimu wa Neno la MUNGU kwa sababu linatupa kuwa na akili; ndiyo maana haachi kulipiga vita ili lionekane halifai. Linda na utunze sana Biblia yako maana kuna hatari ya kupotea baadaye.
Biblia za Udanganyifu
MUNGU ameagiza maana ya maandiko ibaki yeye alivyokusudia, lakini badala yake kuna Biblia zinaitwa zenye tafsiri rahisi; tafsiri za Kiswahili cha kisasa, wakiwa na dhumuni la kusema Biblia ya zamani ni ngumu. Je ndivyo ilivyo?! Jibu ni hapana. Biblia inapaswa kutafsiriwa kama ilivyo kwa utulivu wa akili na uongozi wa ROHO MTAKATIFU. Kabla ya kusoma Biblia lazima maombi kwanza, mazingira ya utulivu na utulivu wa akili ili ROHO wa MUNGU akupe kuelewa.
Huku ni kutegemea akili zako kumuelewa MUNGU; jambo ambalo haliwezekani. Biblia za Tafsiri mpya hazijaandika jina YESU kuwa ni jina la MUNGU na majina mengine ya MUNGU hayajaandikwa; bali jina la MUNGU ni YEHOVA tu. Biblia hii iliandikwa na kufanywa hivyo na Mashahidi wa Jehova. Maana yake ni kupinga kwamba YESU KRISTO sio MUNGU; je huu sio uongo? Ni uongo mtupu.
Ukristo ni dini ya MUNGU ambayo maana kamili ni wafuasi wa YESU KRISTO. Dini hii inaongozwa na kitabu cha MUNGU yaani Biblia; kila kanisa na kila Mkristo imempasa kufuata Biblia kikamilifu.
[5]Kila neno la MUNGU limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio.
[6]Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.
Kwa nini Biblia iwe na vitabu 66 na nyingine iwe na vitabu 72 na wote ni Wakristo?! Biblia sahihi ina vitabu 66. Neno la MUNGU ni hakika na amini; halipaswi kuongezwa wala kupunguzwa na mtu. MUNGU amekataza kwa ukali, laana, na kuzidishiwa mapigo kwa mtu yeyote atakayeongezea Neno la MUNGU.
[37]Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; Kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.
Jambo lolote likizidi katika kiwango au kipimo chake, huwa uongo na udanganyifu; hubeba upotoshaji na hila za kuharibu maisha ya watu kiroho na kimwili. Neno la MUNGU limehakikishwa; hakuna haja ya kuongeza vitu vingine. Ukiongeza maana yake halitoshi; je wewe umemzidi MUNGU maarifa? Jibu ni hapana; kwa hiyo wewe ni mwongo.
[18]Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, MUNGU atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
[19]Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, MUNGU atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
Biblia nyingi siku hizi zimekuja na alama za kishetani na uongo ndani yake. Watumishi wengine wanajua wengine hawajui; halafu ndio wanazitumia kuhubiria madhabahuni. Kwa hali hii watu wengi wanaopotea kwa sababu hawapati maarifa sahihi; wanapata udanganyifu kwa sababu ya Biblia za kishetani. Mikakati ya shetani ipo na Biblia za uongo; ewe Mkristo uwe makini sana na Biblia hizi zilizobadilishwa, ama zilizoongezewa lugha za kisasa.
Watu Wanavyodanganywa na Shetani
[1]Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;
[2]Kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe.
ROHO MTAKATIFU ananena ndani ya Mtume Paulo, kufunua yatakayotokea. Watu kujitenga wao wenyewe na MUNGU kwa kusikiliza roho za shetani. Hauwezi kufanikiwa katika MUNGU pasipo kuifuata imani ya MUNGU. Kwa sababu walio ndani ya imani wanakuwa ndani ya mapenzi ya ile imani. Jambo la kukutenga na MUNGU ni jambo la hatari sana; inakupasa uliepuke kwa sababu litaondoa tumaini lako na kukuzuia kumuona MUNGU.
Kujitenga ni maamuzi ya mtu mmoja, wawili au zaidi waliokubaliana kuacha jambo fulani kwa kujiepusha nalo. Nyakati za mwisho ni nyakati ambazo uovu ni mwingi; wengi wanazidi kufanya mambo ya kuchukiza na kuumiza mbele za MUNGU na wanadamu. Kitu kinachoweza kukutenga na imani sio kitu cha kawaida; ni kibaya sana.
ROHO MTAKATIFU aliyasema haya kupitia Mtume Paulo ili kusudi watakatifu wawe makini. Kwa udanganyifu watu wengi wanaiacha imani ya utakatifu na kuwa waovu. Hebu jiulize na kutathmini; unaishi ndani ya imani au tayari umeshajitenga? Maana kipindi hiki ni nyakati za mwisho zinazosemwa katika maandiko matakatifu. Kwa sababu muda wowote BWANA YESU anaweza kurudi kuchukua watu wake, yaani sisi tunaomwamini.
Mambo Yanayowatenga Watu na Imani
Kwa nini watu wanajitenga na imani? Jibu ni kusikiliza roho zidanganyazo; roho hizo ni roho za shetani, makao yake ni kuzimu, zinashawishi kutenda dhambi na maovu. Anayeongozwa na roho za shetani hutembea katika mapenzi ya shetani na kuacha kufanya mapenzi ya MUNGU.
Kutoka kwenye imani maana yake ni kutolewa kwenye mapenzi ya MUNGU; yaani mambo yote yanayompendeza MUNGU, mtu anaacha kuyafanya. Mtu huyo hawezi kumuona MUNGU maana yuko nje ya MUNGU; atamwonaje MUNGU?
Roho Zidanganyazo
Roho nyingi za shetani zinatenda kazi duniani, lakini kwa Mkristo wa kweli ni lazima ahakikishe kwamba ROHO MTAKATIFU tu ndiye kiongozi wa maisha yake ya kila siku.
[1]Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;
[2]Ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;
[3]Ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.
Maana yake; kuna roho mbalimbali za shetani, zinazotenda kazi ndani ya watu wasiotii maagizo ya MUNGU. Roho hizo ndizo zinazoitwa za udanganyifu ili kuwaweka watu katika maisha ya dhambi, watende mabaya na kupinga wema wa MUNGU maishani mwao. Wanaomuamini YESU KRISTO huongozwa na ROHO MTAKATIFU, yaani Roho wa MUNGU. Lakini watu wasioamini, yaani waliomkataa YESU KRISTO na wale waliomuamini kisha wakamuacha kwa kuikana imani (kuasi) huongozwa na roho mbalimbali za ufalme wa kuzimu.
Roho za uzinzi, roho za uongo, roho za tamaa, roho za mauaji (mauti), roho za hasira na ukatili. Roho hizi hutenda kazi sawasawa na kila dhambi kwa kila roho.
Kujitenga na Imani
Mwanadamu anayeishi bila kumuamini BWANA YESU huongozwa na mwili na matendo ya mwili ndiyo huamua maisha yake. Mtu anayejitenga na imani ni yule ambaye moja kwa moja amekataa kuamini MUNGU anachosema. Kujitenga na imani ni kukataa kuambatana au kukataa kuongozwa na Neno la MUNGU.
[16]Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu?
[17]Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.
Watu wengi wanaabudu miungu kwa sababu ndani ya dunia hii kuna imani nyingi; ila ya kweli ni moja tu, nayo ni kumuamini YESU KRISTO kama Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Biblia imeonyesha miungu mbalimbali inayoabudiwa; zipo sanamu na wapo watu wanaoabudiwa na wamepewa nafasi ya heshima ambayo alitakiwa akae MUNGU tu. Kuna makanisa ambayo wanadamu wamechukua nafasi ya MUNGU kiwango cha kuabudiwa na kanisa. Watu wanawaogopa na kuwaheshimu wachungaji, maaskofu, mitume na manabii wao kuliko hata MUNGU.
[8]Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.
Yaani Neno la MUNGU liseme hivi, mwanadamu aseme hivi; je utamtii mwanadamu kuliko MUNGU? Yaani kuna watu vile ambavyo imewapasa kunyenyekea kwa MUNGU, wananyenyekea kwa wanadamu. Kuna mitume, manabii na wachungaji wanaoheshimika leo kuliko MUNGU; badala ya wawakataze watu wasifanye hivyo, wao wanakubali kupokea utukufu wa MUNGU kwaajili ya nafsi zao.
[9]Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa.
[10]Akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda.
[11]Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu.
[14]Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele,
[15]Wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea MUNGU aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo.
Paulo na mitume walipotukuzwa na wanadamu kiasi cha kuabudiwa kutokana na miujiza MUNGU aliyowapa kufanya, walikataa na kusema hapana; sisi ni wanadamu mpeni utukufu MUNGU. Wajibu wa watumishi wa MUNGU wa kweli; hata kama MUNGU atawatumia viwango vikubwa kiasi gani, bado ni wanadamu tu, hawana sifa ya kuabudiwa kama MUNGU.
[22]Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni MUNGU; hapana mwingine.
[23]Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa.
MUNGU AMEAPA; maana yake MUNGU ameagiza na amedhamiria kwa nguvu zake; ni maagizo, aabudiwe peke yake. Anavyosema kila goti litapigwa kwake ni kwamba hakuna kama yeye, wala tusimwabudu miungu mingine. Magoti haya ni kwaajili ya kumpigia MUNGU tu, sio mwanadamu au vitu. Hata kama duniani kuna imani nyingi, lakini kumuabudu MUNGU kwa njia ya YESU KRISTO ndio imani ya kweli.
Lakini ninakusihi kwamba shika Biblia na uyaishi maandiko matakatifu yaliyoandikwa humo, maana hiyo ndio Neno la MUNGU. Kama sio Neno la MUNGU nisingeweza kuwa hapa leo; maana ndani ya Neno la MUNGU kuna nguvu za MUNGU na neema nyingi zinazoendelea kubadili watu na kuwatengenezea njia ya haki na usalama, nikiwemo mimi.
[16]Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu.
[17]Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye.
Neno la MUNGU ni dira; ukipoteza hili umepotea kabisa njia ya kwenda mbinguni.
Dira ni uelekeo unaokuonyesha wewe uko wapi na unakoenda ili kusudi usipotee.
[22]Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa MUNGU, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele.
Watu wamekuwa watumwa wa watu na sio watumwa wa BWANA YESU. Imani hii ni mbaya na imepotoka yenyewe pamoja na watu wanaoishika. Sisi tunamuamini YESU KRISTO ni watumwa wa BWANA YESU na KRISTO YESU ndiye Bwana wetu yaani kiongozi ambaye akisema kitu sharti tufuate na kutii. Utumwa wa Kristo ni kufuata ya KRISTO na Neno la KRISTO; ukifuata Neno la MUNGU hakuna kudanganywa na kupotezwa na roho za uongo.
UONGO ni kitu hatari, kibaya mno; manabii na mitume wa uongo ni wengi sana. Mimi nimeamua kusema ukweli wote wa injili; zamani nilikuwa huko, nilikuwa miongoni mwa wahubiri wa uongo ndani ya chama cha mitume na manabii. MUNGU alinipa neema ya kutoka huko. Hata kama ni gharama kuusema ukweli, lazima iwe hivyo. Inanipasa kugharamia ukweli kama BWANA YESU KRISTO alivyoagiza ili niingie mbinguni.
Kupenda Fedha
Shetani amefanya watu kupenda sana fedha ili wasimuone MUNGU. Hii ni mbinu moja wapo na mtego wa kunasa watu wengi hata wateule wa MUNGU. Maisha yanapokuwa magumu ni namna ambayo MUNGU ameruhusu wakati mwingine kama mapito na kipimo cha imani. Wakristo wengi wameshindwa kuvumilia changamoto ya njaa na umaskini; wamedanganywa na kuiacha imani ya kweli, hawana YESU tena mioyoni mwao.
[8]Ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.
[9]Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.
[10]Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.
Udanganyifu ambao Shetani amepandikiza kwa watumishi wa uongo, ambao wengine walikuwa wa kweli ni kupenda fedha; kwa sababu hiyo wameiacha imani. Wanafanya miujiza ya uongo na maigizo kwa msemo halisi mazingaombwe; yaani hakuna ukweli.
Miujiza na Ishara
Wateule wengi hawajui miujiza sio msingi wa injili bali kweli ya wokovu katika YESU KRISTO. Kama wanajua basi changamoto zimewafanya wasahau. Kwa njia ya miujiza shetani amewapoteza Wakristo wengi waiache imani na kufuata mafanikio tu.
[1]Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,
[2]Ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;
[3]Wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa BWANA, MUNGU wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda BWANA, MUNGU wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.
[4]Tembeeni kwa kumfuata BWANA, MUNGU wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.
Watu hawajui kwamba miujiza sio maana kuu ya kuzingatia; miujiza sio ishara kuu ya imani. Yaani kutendeka kwa miujiza sio kigezo cha kusema imani fulani ni sahihi. MUNGU ameweka wazi kwamba tuwe waangalifu kuyatazama sana maagizo ambayo ametupa na kuyafanya. MUNGU alisema hivi kwa sababu shetani naye anaweza kutenda miujiza. MUNGU ni Tajiri wa utukufu; hakumnyanganya shetani uwezo na nguvu wala wale malaika wengine walioasi.
Kujua Miujiza ya MUNGU
Miujiza ya MUNGU lazima iwe mikubwa kama ikilinganishwa na ya shetani; hata kama isipokuwa ya kutisha sana lengo kuu ni kuwavuta watu kumuamini YESU KRISTO. Lakini kingine ni kwamba miujiza ya MUNGU haipo katika kuamini vitu viitwavyo vya Upako bali jina la YESU KRISTO, pamoja na badiliko la tabia yaani watu kuacha maisha ya dhambi na kuwa wema.
Hata kipindi kile Musa alipokuwa ameagizwa na MUNGU kuwatoa wana wa Israel utumwani, alipewa matendo ya miujiza kama ishara ya kuaminika kwa Waisraeli na mbele ya Farao. Lakini wachawi nao walifanya miujiza kama namna ya kumjibu Musa kwa nguvu za shetani ili kuzuia kusudi la MUNGU.
[10]Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka.
[11]Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.
[12]Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.
[13]Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama BWANA alivyonena.
Unaweza kujiuliza; kwa nini wachawi na wao walifanya miujiza? Lakini MUNGU hakuzuia fimbo zao zisiwe nyoka kama fimbo ya Haruni. Shetani hufanya miujiza ili kuangusha imani; watu wasimzingatie MUNGU. Kwa kuwa wengi wanapenda miujiza wamedanganywa; wanasahau umuhimu wa Neno la MUNGU, hawalisomi, badala yake wameingia kuamini vitu badala ya MUNGU.
Zamani manabii wa uongo waliuawa baada ya kugundulika kwa sababu ilikuwa jino kwa jino katika agano la kale; watu waliongozwa na Torati. Leo hii manabii wa uongo wanapojulikana kuuawa kwao ni watu kuacha kuwafuatilia kwa sababu tupo rohoni. Manabii wa uongo wanapata nguvu za kuendelea kwa sababu ya idadi kubwa ya watu wanaowapigia. Nabii wa uongo akiendelea kuishi ataleta madhara makubwa kwa kuzidi kupoteza watu. Kwa hiyo kipindi cha Torati waliuawa. Nabii Eliya alimtukuza MUNGU dhidi ya Baali; akawachinja manabii wa uongo wote ambao walisema Baali aabudiwe, kwa sababu agizo lilitolewa na MUNGU wauwawe.
[38]Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.
[39]Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye MUNGU, BWANA ndiye MUNGU.
[40]Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko.
Kisa cha Nabii wa Uongo Redioni
Wakati mmoja hivi; kuna kituo kimoja cha redio cha masafa ya FM niliwahi kwenda pale kutembelea, ni hapa hapa Tanzania. Nilipofika nilikuta muda wa kipindi; amerusha Nabii mmoja hivi, kila siku huwa ni ratiba yake muda huo kurusha kipindi. Yaani kama vile yuko palepale muda huo anahubiri yaani mubashara redioni; kisha anaombea watu na baadhi ya watu wanashuhudia jinsi wameponywa shida na magonjwa yao mubashara.
Lakini yule Nabii hakuwepo; alikuwa amerekodi mahubiri yake na amewapa flash watu wa redioni; wao wameweka inaongea lakini yeye hayupo. Nikawaambia mbona mnafanya huu utapeli, mbona mnashiriki uovu? Yule Nabii alikuwa anaweka simu yake bize; watu wapige simu kuombewa lakini namba yake ya simu inaonyesha anawasiliana na mtu mwingine, kisha anawaambia watume sadaka. Ni uongo mtupu huu.
Nilipowauliza kwanini watu wa redioni wanakubali hayo, wakasema "manabii hao hulipa pesa nyingi, ni faida kwetu, sisi tunaangalia; hata wewe tunaweza kukufanyia hivyo". Nikakataa; hiyo ni dhambi, ni uongo na utapeli. Nilipowauliza kwanini msiache kupokea pesa za hila na utapeli kama huu, wakasema kuendesha vipindi ni gharama; inatakiwa tupate faida na tuwalipe wafanyakazi wa hapa redioni. Wanafanya hivyo wasijue kuwa na wao wanashirikiana na shetani kufanya kazi ya udanganyifu.
Katika hukumu, manabii wa uongo, wamiliki wa redio zenye kuwatangaza manabii wa uongo, na wasikilizaji wote wamehesabiwa hukumu moja kwa sababu wametenda kazi moja na shetani na kupoteza watu. Kwa sababu kama sio redio watu wasingesikiliza huo uongo wakapotea.
Watu wengi wameingia kwenye udanganyifu bila kujua. Chunguza uone jinsi ambavyo watu wengi wanafuatilia redio na vipindi vingapi katika runinga vinavyorushwa na manabii wa uongo. Wamezama kwenye mafundisho ya uongo wanasikiliza roho zidanganyazo; maana hakuna ukweli katika utapeli, hakuna ukweli wenye uongo ndani yake. Hata kama watumishi hao wanatumia Biblia, utapeli wanaoufanya na miujiza ya uongo sio ukweli tena; ni udanganyifu.
[14]Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?
[15]Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?
Manabii Wengi Sio Watumishi wa MUNGU
Ndio maana wameweka viwango vya pesa, tena viwango vikubwa tu; yaani ukitaka huduma kwao manabii na mitume hawa, unalipia kwanza na bila kulipia pesa hizo haupati huduma uliyotaka kutoka kwao. Shetani anatumia sana watumishi wanaojifanya kuwa wa kweli ili kuwafanya watu wengi wapotee hasa wale waliamini.
Kumuona Nabii: shilingi 300,000
Kununua maji: shilingi 10,000 kwa chupa moja
Mafuta: shilingi 20,000
Kushikana mkono na Nabii au Mtume: shilingi 70,000
Haya yote yanatokea kwa manabii na mitume wa namna hii; hawamtumikii MUNGU bali wanafanya biashara na uongo ambao shetani amewatuma kupoteza maisha ya watu wanaomwamini YESU KRISTO.
Je, BWANA YESU KRISTO alifanya hivi katika maandiko? Aliagiza nini kifanyike ili kuwahudumia watu kiimani, wanaotaka uponyaji? Tuone maandiko matakatifu:
[7]Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.
[8]Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.
Tunaona kumbe BWANA YESU alisema tufanye maombezi kwa watu wote bure; matajiri au maskini. Akaagiza tusipendelee wala kuangalia pesa, cheo, nafasi au mwonekano wa mtu; bali wote kuwaona kama watu wa MUNGU wanaohitaji msaada.
[1]Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.
[3]Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.
[11]Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu.
Kupata mapato ya aibu ni kupata fedha au mali kwa njia zenye uovu na dhambi. Kazi yoyote ambayo haimpendezi MUNGU haupaswi kufanya ewe mwanadamu. Fahamu kwamba kupata pesa wala mafanikio sio shida; ila ni kwa njia ipi? Ni njia inayowezesha au kurahisisha waovu kuwa waovu zaidi au ni njia ya haki?
Ushuhuda Mfupi
Siku moja mama mmoja aliyekuwa muuza baa alikuwa anasali kanisani kwa Nabii mmoja hivi. Kumbe yule Nabii alikuwa na tabia ya kwenda kupata pombe katika baa hiyo ambayo yule mama huwa anauza. Yule Nabii alikuwa anavaa kofia ya kufunika uso ili asijulikane; alafu anapokunywa bia huinamia chini kofia imfunike sura yake.
Siku moja yule mama akawa anadai chenji akainama hivi; kumbe ni yule Nabii. Akaanza ugomvi "nirudishie pesa yangu niliyokupa sadaka". Ilikuwa ni ugomvi mkubwa sana.
Ndege wafananao huruka pamoja. Yaani kanisa lenye udanganyifu na kuruhusu uhuru wa maisha; mchungaji hawezi kuwa salama! Mafundisho yasiyoleta mabadiliko ya tabia na mienendo ya watu; mchungaji wa kanisa hilo lazima awe na michanganyo. Wachungaji, maaskofu, mitume na manabii wengine hawajaokoka; hata kama waliokolewa basi waliacha imani na kufuata mambo mengine. Pesa, uzinzi na umaarufu vimewaangusha dhambini bila watu kujua.
Manabii wa Uongo Kuingia Madhabahuni
[10]Huyo mtesi amenyosha mkono wake juu ya matamaniko yake yote; Maana ameona ya kuwa makafiri wameingia ndani ya patakatifu pake; Ambao kwa habari zao wewe uliamuru wasiingie katika kusanyiko lako.
Shetani ameweka mkono wake juu ya kanisa; anatenda kazi kwa nguvu na bidii, anafanya kila anayotaka kwa sababu mawakala yaani manabii na mitume wake wa uongo wanasimama madhabahuni. MUNGU alikataza tangu agano la kale (kipindi cha Torati) manabii wa uongo wasiingie madhabahuni. Anachokifanya shetani ni kuwapa mafundisho ya uongo ambayo yamelenga kupoteza Wakristo. Anafanya kuliondoa tumaini la Wakristo kwa YESU; waweke tumaini katika vitu.
Kanisa tunamhitaji ROHO MTAKATIFU kila wakati; hasa katika muda huu tuliopo ni hatari sana kwa sababu uongo ni mwingi. Kama ROHO MTAKATIFU alivyoyafunua haya; waongo wote anawajua. Tunahitaji kuongozwa naye ili atufunulie wote wa kweli. Muulize akupe kujua wadanganyifu ulionao katika maisha yako. Pengine ni mchumba wako, rafiki yako, na mtu yeyote yule wa karibu amebeba hila za kukuua. Pata muda uombe na ROHO MTAKATIFU atamfunua kwako.
Roho za Udanganyifu Zinavyotenda Kazi
MUNGU ameweka uongozi kama mfumo wa utawala kama ilivyo mbinguni. Mchungaji wa kanisa akitenda wema kama MUNGU alivyoagiza katika Neno lake basi ni MUNGU amesema kupitia huyo kiongozi. Mchungaji, askofu, mtume ndio waangalizi wa kanisa; imewapasa kuongoza kanisa na sio waumini ndio waongoze kanisa. MUNGU hapangiwi na malaika cha kufanya; hivyo waumini nao wasimpangie mchungaji ya kuhubiri; MUNGU aongoze kanisa kwa Neno lake kupitia Mchungaji.
[9]Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA;
[10]Wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo;
[11]Tokeni katika njia, geukeni mtoke katika mapito; mkomesheni Mtakatifu wa Israeli mbele yetu.
Watu ndio wanaamua nini kihubiriwe na wanampangia mchungaji cha kuhubiri; kama sivyo hawaji kanisani. Watumishi wengi wanatii washirika wao kwa kuogopa wasipungue kanisani; kwa hiyo wanahubiri mapenzi ya washirika. Lakini hawajui kuna hukumu kuhubiri mapenzi ya watu na kuliacha Neno la MUNGU. Idadi kubwa ya watu muda wa ibada sio ukubwa wa kanisa. Kwa Wakristo kila kitu hupimwa namna MUNGU anavyotaka; kipimo cha MUNGU ni utakatifu yaani ukamilifu wa kufuata Neno lake linavyosema.
Kanisa kufanana na dunia ni kanisa kuishi kama dunia na mitindo ya kidunia; hii huitwa chukizo la uharibifu. Chukizo la uharibifu ni mambo yanayozuia mtu mwenye juhudi za utakatifu asifike kiwango; watu wasimuamini YESU KRISTO na injili isihubiriwe sawasawa. Haya yanapofanyika kanisani ni moja kati ya ishara za kurudi kwa BWANA YESU. Katika hili ndipo tunajua sifa mojawapo ya kanisa la kweli ni kutokufuata mifumo na taratibu za kidunia.
[9]Akasema, Enenda zako, Danieli; maana maneno haya yamefungwa, na kutiwa muhuri, hata wakati wa mwisho.
[10]Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndio watakaoelewa.
[11]Na tangu wakati ule ambapo sadaka ya kuteketezwa ya daima itaondolewa, na hilo chukizo la uharibifu litakaposimamishwa, itapata siku elfu na mia mbili na tisini.
Ni juhudi zote za shetani kukwaza imani; kuzuia utakatifu usipatikane kwa Wakristo. Jambo chukizo ni kitu kibaya au jambo lenye kuudhi, kukwaza, kuangusha na kuua imani ya utakatifu katika YESU KRISTO. Haya ndiyo yamekuwa ya kawaida katika kanisa la leo; yanafanyika kwa uwazi kabisa na wachungaji wengi wamechukuliana nayo pasipo kufanya namna ya kuyaondoa.
MUNGU Huyachukia Mambo Haya
Dhambi ni kitu au jambo kinyume na maagizo ya MUNGU; ni upagani na udunia; yaani kawaida ambazo watu wa dunia (wasioamini) wanafurahia. Watakatifu ni wacha MUNGU; huchukia dhambi.
Njia kuu ya mwenye haki ni kujitenga na uovu; Yeye ashikaye njia yake huihifadhi nafsi yake.
Ni jumla ya mafundisho yasiyomtukuza YESU; bali mafanikio, utajirisho, maji, mafuta na upako wa vitu. Mafundisho hayo hayazungumzii kazi ya msalaba ya ukombozi na wokovu kwa mwanadamu. Lakini pia mafundisho ya mpinga Kristo hayazungumzii kabisa ujio wa YESU KRISTO kuchukua kanisa lake bali mambo ya ulimwenguni; mambo yenye kuwapotezea muda watu wadhani kuwa maisha ya duniani yana umuhimu kuliko ya milele mbinguni.
MUNGU anataka tuwe kama yeye kwa tabia na mwenendo; maana kwa sura sisi ni mfano tu, yeye ni mtukufu sana hatufanani naye. Mhubiri anayewafurahisha waovu, asiyebadili tabia za waovu kuwa wema kwa mafundisho anayotoa ni mdunia; hafai, kuna udanganyifu ndani yake. Filamu tamthilia, mpira wa miguu, disko, klabu, fasheni; haya ni mambo ya dunia. Watu wa dunia huyafurahia lakini kwa watakatifu ni machukizo ya imani.
[5]Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia.
[6]Sisi twatokana na MUNGU. Yeye amjuaye MUNGU atusikia; yeye asiyetokana na MUNGU hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu.
Kwa mfano mhubiri anayesema njoo mtu wa dini yoyote, anafanya maombi ya uponyaji bila mafundisho ya imani, badiliko la mienendo na utakatifu; huyo sio wa MUNGU ni wa dunia; yuko kwenye biashara. Kwa mfano pia mhubiri anayesema kila mtu aende kanisani anavyotaka, kwa mavazi na mitindo yoyote bila badiliko; huyo ni mdunia hafai, ni wakala wa shetani kwa njia ya udanganyifu.
[15]Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;
[16]Kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.
Maneno laini ya kupoteza huhubiriwa na manabii wa uongo; kusudi lao ni kupoteza watu wa MUNGU wasitembee katika dira ya utakatifu. Kusudi kuu la manabii wa uongo ni kuwafanya watu wajisahau; wasijali juu ya utakatifu na safari ya kwenda mbinguni yaani wawaze tu ya duniani.
[17]Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao.
[18]Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu.
Ratiba na mwenendo wa ibada; ibada zinazofanyika kwa mfumo wa kipagani na udunia hazitakiwi. Udanganyifu mwingine wa shetani ni kuingiza mambo ya kidunia na ushetani mpaka kanisani; kwenye ratiba za ibada. Siku hizi nyimbo za kidunia, midundo na uimbaji wa kidunia, unyoaji wa nywele na fasheni za mavazi; hapo MUNGU hawezi kuwepo na kanisa litaelekea kuzimu.
[27]Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za MUNGU Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.
Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.
Shetani hapendi ukweli; kwa hiyo anapiga vita sana injili ya kweli.
Ni mapambano ya vita na kujipa moyo katika YESU KRISTO, nikiiamini kuwa nitashinda.
Usidhani kuwa ni rahisi kuhubiri injili ya kweli; ni hatari mno.