UTANGULIZI
Historia yake
Paulo ni mwalimu, mtume, mwinjilisti na Myahudi ambaye jina lake la kwanza, la Kiyahudi lilikua Sauli, ambaye Bwana Yesu alimfanya chombo kiteule chake, ili alichukue Jina lake mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Alizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, na kupelekwa Yerusalemu, akafundishwa Torati kwa usahihi miguuni pa Gamalieli, ambaye ni Farisayo aliyekua maarufu sana wakati huo (Mdo 22:3) Alikua na ujuzi wa ufundi wa kutengeneza na kushona mahema (Mdo 18:3). Jina Paulo, ni jina la Kirumi (Latin. ‘Paullus’) ambalo lilikua jina la mbadala kwa sababu alikua na uraia wa Kirumi na Kiyahudi, na ndilo lilimsaidia sana katika kueneza Injili katika miji aliyokua akieneza Injili kwasababu ilitawaliwa na Warumi (Mdo 13:9).
Mateso kwa Kanisa
Paulo aliliharibu, kulitesa na kuliudhi kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani, akiwafunga, hata kwenda kwa Kuhani Mkuu na wazee wa baraza na kupokea barua na kupita miji kwa miji ili awalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe (Mdo 8:3; Gal 1:11). Alishiriki katika kifo cha mfia dini, Stefano naye ‘aona vema kwa kuuwawa kwake’ kwani ndiye aliyeshika nguo za wale waliomwua Stefano (Mdo 7:58; 22:20).
Kuongoka
Alitokewa na Bwana Yesu akiwa anaelekea mji wa Dameski (Mdo 9:1-8) na kupewa mafunuo (Gal 1:11-12) kwa ajili ya kufanya kazi ya Bwana, akatiwa upofu, akakaa siku tatu bila kula wala kunywa, kisha akawekewa mikono na Anania na kutolewa upofu, kisha kubatizwa. Akaelekea Arabuni, kisha akarudi Dameski na kukaa siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi, akihubiri Injili (Mdo 9:19; Gal 1:17).
Mchango wa Mt. Paulo katika Kanisa la Kwanza.
Mwalimu wa Neno la Mungu.
Kanisa la Antiokia
Paulo, kabla ya kutengwa na Roho Mtakatifu kuwa mtume wa mataifa, alikua mmoja kati ya walimu na manabii waliokuwapo katika Kanisa la Antiokia (Mdo 13:1); kwakuwa alikua amefundishwa Torati na Rabi Gamalieli, basi alikuwa msaada katika kufafanua maandiko na kuyaoanisha na Injili katika Kanisa la Kwanza.
Masinagogi na Makanisa ya utawanyiko.
Mtume Paulo alikua na desturi ya kuingia katika masinagogi ya Kiyahudi, katika kila mji alipokwenda kuhubiri, hivyo ilimpasa ajue vizuri torati na kujua kuifafanua kwa wale ambao ni Wayahudi, na hata wakati mwingine kwa Wayunani. Hii inadhihirishwa sana alipokuwa mji wa Thesalonike, kwani aliingia na “akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu, akiyafunua na kuwaeleza ya kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya kwamba, Yesu huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo.”(Mdo 17:2-3).
Injili kwa Mataifa
Paulo alipokuwa Yerusalemu, akisali ndani ya Hekalu, Bwana Yesu alimtokea, akamwagiza akahubiri kwa Mataifa (Mdo 22:18-21), pia akiwa Antiokia pamoja na wanafunzi wengine, wakifunga na kuomba, “Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.”(Mdo 13:2b). Kwani “(ali)kabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa”(Gal 2:7).
Paulo, kwa ujasiri na msaada wa nguvu za Roho Mtakatifu alihubiri katika miji mingi ya Asia ndogo pamoja na Ulaya akishirikiana na Barnaba, Sila, Timotheo, Tito, Akila na Prisila na wengine. Alipita katika miji ya Kipro (Salami na Pafo); Pamfilia (Perge); Pisidia (Antiokia); Likaonia (Listra, Derbe); Troa; Makedonia (Filipi); Thesalonike; Korintho; Ugiriki (Athene); Efeso; Rumi n.k. (Mdo 13-21)
Kuanzisha Makanisa mapya.
Paulo alifanya safari tatu za kiuinjilisti na katika safari hizi aliweza kuanzisha makanisa katika kila mji alioupita. Katika miji yote iliyotajwa hapo juu, alihubiri Injili kwa ushujaa, kwa “ishara na maajabu ambayo Mungu aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa.” (Mdo 15:12). Katika kuhubiri kwake, “wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi…”(Mdo:19:9). Hivyo kwa waliokataa aliwaacha, na kuwatenga wanafunzi, na hao ndio waliokuwa mwanzo wa makanisa katika miji mbalimbali.
Ashiriki Baraza la Kwanza la Yerusalemu
Baada ya Wayahudi kutoka Yerusalemu kuwafundisha Wakristo wa mataifa ya kwamba, wasipotahiriwa kama desturi ya Musa hawawezi kuokoka (Mdo 15:1), Paulo na Barnaba walilazimika kwenda Yerusalemu, wakisafirishwa na kanisa, ili kujadili mjadala huo. Kuhusu jambo hilo, kwa hekima ya Petro, Paulo, Barnaba na Yakobo, lilitatuliwa na kutolewa suluhu na maamuzi kwa moyo mmoja. (Mdo 15:1ff)
Kupitia mtaguso uliotolewa na baraza hili (Mdo 15:23-29), ndipo thelojia ya ‘(tu)meokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi ze(tu), ni kipawa cha Mungu;wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.” (Efe 2:8-9;
Gal 2:16) ilipoonyesha uimara wake kama msingi mkuu wa Kanisa la Kikristo. Tatizo liloibuliwa na Wayahudi lilikua na hatari ya kulitenganisha kanisa na bila shuhuda za jinsi Mungu alivyotenda kazi kwa watu wa Mataifa kupitia Paulo na Barnaba, pengine kanisa lingegawanyika.
Kuimarisha Makanisa na kuteua Waangalizi (Maaskofu)
Baada ya kuanzisha na kuwatenga wanafunzi katika miji aliyohubiri, Paulo na Barnaba, walirudi katika miji ile, “wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani …” (Mdo 15:22).
Paulo akishirikiana na Barnaba, “waliwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini” (Mdo 14:23). Moja wa viongozi hawa walikua Timotheo, Tito pamoja na Akila na Prisila. Hawa wote aliwaasa watunze nafsi zao, na kuwalisha kundi lote lililoko chini yao, . (Mdo 20:28).
Barua kwa Makanisa na kwa Wachungaji
Nyaraka alizoziandika Mtume Paulo kwa makanisa ya Rumi, Galatia, Thesalonike n.k pamoja na kwa wachungaji (Timotheo na Tito), ni hazina kubwa sana ambayo Roho Mtakatifu, kwa kupitia Paulo, aliziacha kwa ajili ya kukuza uelewa na theolojia yetu kuhusu Injili na Mungu kwa ujumla. Paulo aliandika nyaraka takribani kumi na tatu (13), zilizoweza kuhifadhiwa hata sasa na kuwekwa katika Biblia.
Roho Mtakatifu alimtumia Paulo kusema na kanisa na kudhihirisha kweli halisi kwakuwa nyaraka hizi ni Neno la Mungu, nazo zikawa funguo za kuonyesha ukweli kuhusu Kristo kwa mataifa. Zilionyesha ukomavu wa Paulo katika imani yake, na hivyo kuwa kielelezo kizuri kwa Kanisa la Kwanza na hata kwa vizazi vyote vilivyofuata, kwani nyaraka hizi ni wazi ziliandikwa kabla ya Injili kuandikwa, na kusomwa katika makanisa ya kipindi hicho.
Mambo ya kujifunza kutokana na maisha na utumishi wa Mt. Paulo.
Mwinjilisti wa karne hii ya ishirini na moja, anayo mengi sana ya kujifunza kutokana na maisha na utumishi wa Mt. Paulo. Baada ya kujifunza kupitia maagizo ya Bwana Yesu Kristo, mfano pekee wa kuiga na wa kielelezo wa namna ya kuyaishi maisha yaongozwayo na roho, haswa kwa mtu ambaye hakuwa na Uungu kama Yesu, ni maisha ya Mtume Paulo. Naye asema, ‘mnifuate mimi kama mimi nilivyomfuata Kristo’ (1 Kor 11:1). Yafuatayo ni mambo ya msingi ya kujifunza;
Neema ya Mungu ni ya kipekee.
Ingawa Paulo (Sauli) alilitesa na kuliudhi kanisa sana hapo mwanzo, neema ya Mungu ilimwinukia na kumbadilisha toka chombo cha uharibifu, na kuwa chombo cha utakatifu. Nguvu hii ya Mungu ndiyo neema yake, ambapo ilimstahilisha pasipo yeye mwenyewe kustahili.
Hili likawa funzo na mkazo wake mkubwa sana katika Injili na mahubiri yake, ikionyeshwa wazi katika nyaraka zake kwa Warumi na Wagalatia, nayo kumvuta kusema, “ Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.(Efe 2:8-9). Hivyo tutambue kwamba hata sasa Mungu anaweza kuwaokoa watu hata wanaolitesa au ni wapinzani wa Kanisa, hata wale ambao ni waovu wakubwa ambao hawadhaniwi kwamba waweza kuokoka, mfano wachawi, wezi, wauwaji na hata waganga wa kienyeji.
Kufunga na kuomba: nyenzo muhimu kuliko zote katika kanisa na utumishi.
Baada ya Sauli kutokewa na Bwana Yesu na kupewa maono makubwa, alikwenda Dameski na alifunga bila kula wala kunywa (Mdo 9:9) Hii ilikuwa ili kumtayarisha kwa ajili ya huduma yake ya kufanya utume kwa mataifa. Nasi kama tukitaka huduma yetu iwe na nguvu za Mungu, ni vyema kufunga na kusali.
Kabla ya Roho Mtakatifu kumtenga Paulo na Barnaba, mitume walikuwa wanafunga na kuomba (Mdo 13:2-3). Hii ilisaidia katika kuachilia Roho Mtakatifu awe nyenzo kuu katika kukuza Kanisa lake. Nasi tunapotaka Mungu afanye huduma kubwa naya kipekee katika Kanisa la sasa, ni vyema tufunge na kusali.
Kabla ya kuwawekea mikono wazee na waangalizi wa makanisa ya Listra, Derbe na Antiokia ya Pisidia, Paulo na Barnaba walifunga na kuomba (Mdo 14:23. Hii ilisaidia kuhakikisha kwamba viongozi waliochaguliwa, hawakua kwa hekima na mtazamo wa wanadamu bali walitegemea Roho ndie awasimike. Hata sasa ni vyema kufunga na kuomba kama twataka kusimika kiongozi katika Kanisa, ili Roho Mtakatifu afanye kazi hiyo.
Paulo alisisitiza katika barua zake kwamba alifunga na kuomba sana ili kupata nguvu ya kuendelea kuhubiri injili.
Kuwekewa mikono au kusimikwa – Kutengwa kwa ajili ya kazi ya Injili.
Baada ya Roho Mtakatifu kuwatenga Paulo na Barnaba, mitume, “wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.” (Mdo 13:3). Hii ilionyesha kupokea baraka zote kutoka kwa viongozi wa juu ili kufanya huduma.
Baada ya kuanzisha makanisa huko Galatia “na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini.”(Mdo 14:23). Hivyo nao viongozi walioteuliwa na Paulo na Barnaba walisimikwa na kuwekewa mikono.
Kusimikwa huku na kuwekewa mikono humaanisha, hao waliotengwa kwa ajili ya huduma, wamepokea baraka na neema zote kutoka kwa Mungu, kupitia viongozi waliopo. Hata sasa ni vyema kwa mtumishi wa Mungu, kupitia hivyo na sio kama manabii wa uongo wanaoibuka kila siku na kuwalaghai watu.
Mafunzo na mafunuo ya KWELI hutoka kwa Yesu Kristo, sio wanadamu.
Paulo aliwajulisha Wagalatia kwamba, “injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.(Gal 1:11-12). Japo Paulo aliijua Torati sana na kufanya bidii, elimu na bidii yake haikuweza kumleta katika Injili, bali Roho wa Mungu ndiye aliyempa.
Hakuna mwanadamu awezaye kwa maneno yake kutuvuta kwa Mungu, bali Yesu asema waziwazi, “hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.” (Yn 6:65)
Ujasiri wa kuhubiri Injili
Mtume Paulo ni mfano wa kuigwa kabisa kwa namna alivyokuwa jasiri katika kuhubiri Neno la Mungu kwa mataifa. Alinena kwa ujasiri katika masinagogi ya Wayahudi, katika kila mji alioutembelea, mbele ya makadhi na viongozi wa miji, mbele ya askari wa Kirumi, Liwali wa Kirumi, Festo na hata mbele ya Mfalme Agripa.
Hata mtumishi wa leo, yampasa kuwa jasiri katika kuhubiri hata kama ni mbele ya watu wakubwa wa kiserikali bila kuogopa cheo cha mtu wala nafasi aliyonayo; kwani Bwana alisema, “kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.” (Mt 10:32)
Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.
Huu ndio ujumbe aliowapa kwa maonyo na kuwaimarisha Wakristo waliokuwa katika makanisa ya Galatia, baada ya yeye pamoja na Barnaba kupitia katika “taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi.” (2 Kor 11:27)
Mtumishi wa kipindi hiki lazima ayakumbuke maneno ya Bwana kwamba, “Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” (Yn 16:33b). Tusiwe kama mbegu iliyopandwa kwenye miamba, ambapo dhiki ikitokea juu ya Neno la Mungu, huliacha; bali tuwe kama Paulo, udongo mzuri ambapo mbegu ilipopandwa ilikua na kuzaa matunda mengi.
Kufundisha, kulea na kuimarisha wanafunzunzi wachanga katika imani.
Baada ya kuanzisha makanisa katika miji yote, Paulo alimwambia Barnaba, “turejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani.” (Mdo 15:36b). Paulo aliwathamini waongofu wapya katika Kristo, na hii pia hushuhudiwa kwa nyaraka zake kumi na tatu, ambazo humo huonyesha kujali, kufundisha, kuonya na mwendelezo wake wa kuwakuza kiroho wale aliotaabika kwa ajili yao.
Mtumishi hasa mwinjilisti, yampasa kurudi na kuwalea kiroho wanafunzi wale ambao aliwapata katika Injili kwa njia ya semina, warsha na mafundisho mbalimbali. Hii imepungua sana kwani siku hizi tunaona mikutano ya Injili lakini semina chache pamoja na ufuatiliaji hafifu sana kwa wale walioongoka baada ya mikutano ya Injili.
Kulijua Neno la Mungu vizuri na kutambua walengwa wasikiao Injili.
Kujua Neno la Mungu
Paulo alijua sana Agano la Kale, na hii yadhihirishwa kwa namna kila alipoingia katika masinagogi na kunukuu mara nyingi na kwa usahihi Maandiko matakatifu. Hivyo mtumishi lazima kuyasoma, kuyatafakari na hata kuyakariri maandiko ili yaweze kumsadia kuhubiri kwa usahihi na umakini bila kuyumbishwa.
Walengwa wasikiao Injili
Akiwa kwa Wayahudi, Paulo alitumia vizuri Torati na Manabii kuwaelezea kuhusu Yesu, lakini alipokuwa na Wayunani, mjini Athene, alibadilika na kutumia mazingira yao, na taratibu zao ili kufikisha Injili – kupitia ‘Mungu Asiyejulikana’ (Mdo 17:23). Pia alipokuwa katika miji ya Likaonia, baada ya watu kudhani yeye ni mungu, alifafanua kuhusu Mungu kupitia ‘mafunuo ya kawaida’ au ‘general revelation’ kama msingi wa kuhubiri Injili.
HITIMISHO
Yapo mengi sana ya kujifunza kupitia utumishi na maisha ya Paulo ambayo hayawezi elezewa hapa yote, lakini mausia yafuatayo yatosha kujua juhudi zake katika kumtumikia Mungu;
“Lakini mambo yale
yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara
kwa ajili ya Kristo.
Naam,
zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa
ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu,
Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote
nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane
katika yeye,
nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile
ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa
Mungu, kwa imani; ili nimjue
yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake,
nikifananishwa na kufa kwake; ili
nipate kwa njia yo yote kuifikia
kiyama ya wafu. Si
kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali
nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake
nimeshikwa na Kristo Yesu.”
Flp 3:7-12
AMEN
_________________
Vitabu Rejea:
Swahili Union Version, Biblia Takatifu, 1997
Don Fleming, Kamusi ya Biblia, 2016
London, The Inter-Varsity Fellowship, The New Bible Commentary, 1958
www.wikipedia.com, Free Wikipedia, 2019
