UTANGULIZI
Apolo alikuwa mmoja wa watumishi hodari sana katika Kanisa la kwanza, aliyetokea mji wa Iskanderia (Alexandria) – Misri. Alifanya utumishi na huduma yake kipindi kimoja na Mtume Paulo haswa katika makanisa ya Efeso na Korintho. Prisila na Akila walikuwa wenyeji na watumishi wa Mungu waliofanya huduma katika miji hiyo – Mdo. 18:1-2
Walikuwa na uhodari kwa pamoja katika kazi hii hata Paulo alisema kuwa yeye pamoja na Apolo ni mfano wa kuigwa kwa Wakorintho (1Kor. 4:6
Paulo na Apolo walikuwa na uhodari katika kazi ya Mungu kiasi kwamba baadhi ya watu au makanisa yaliyo Korintho kugawanyika kila moja likitaka kuambatana na mmoja wapo (1Kor. 12; 3:5-6
Paulo alipanda Neno la Mungu(mahubiri) kwenye shamba la Korintho, kisha Apolo akafuata na kumwagilia maji (mafundisho) – 1Kor. 3:6
Alikuwa mmoja wa watenda kazi ambao Paulo alipenda kuwa karibu naye sana – Tit. 3:13
MAMBO YA KUJIFUNZA
Katika Maandiko tuliyoyasoma leo, Mungu anataka ujifunze jambo moja kubwa sana kutoka kwa Apolo alipokuwa analitumia Neno la Mungu kama silaha ndani ya huduma yake.
TENGENEZA UHODARI KATIKA MAANDIKO KAMA SILAHA YA KUSHINDA UPINZANI KWA KUKUBALI KUFUNDISHWA KWA USAHIHI NJIA YA BWANA
Uhodari katika maandiko ni kuwa na nguvu au uwezo katika Roho Mtakatifu, wa kutumia vizuri Neno la Mungu ili kujenga au kubadilisha imani au mtazamo wa watu ili umwelekee Yesu Kristo.
Kuweka bidii na juhudi mahususi katika kusoma na kujua maandiko pasipo ulegevu. (kusoma Biblia yote, mstari kwa mstari, mlango kwa mlango, ukurasa kwa ukurasa)
Kuwa tayari na si tuu kujua, bali na namna ya kulitumia Neno la Mungu katika mazingira yote, watu wote, vitu vyote na mahali popote katika mazungumzo na matendo yako.
Kujua maana ya Maandiko; namna ya kutumia Maandiko; namna ya kufikiri kwa kutumia Maandiko; namna ya kushawishi mtu kwa Maandiko; namna ya kutumia mamlaka iliyoko katika Maandiko;
Kupenda elimu na kujifunza ni tabia ya msingi ili kupata uhodari katika maandiko
Moja ya sifa ya Apolo ilikuwa ni mtu wa elimu.
“Moyo wake mwenye hekima hufundisha kinywa chake; Huzidisha elimu ya midomo yake.” – Mit. 16:23
Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima, Ikiwa hana moyo wa ufahamu? – Mit. 17:16
KWANINI UNAHITAJI UHODARI KATIKA MAANDIKO?
Kwanza, ni kusudi la Mungu uwe na uwezo huu
Kabla ya Apolo kuanza kufundisha, Mungu alikuwa amekwisha weka ‘uhodari katika maandiko’ ndani yake. (24)
Kol. 3:16 - Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote
2 Tim. 2:15 - Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.
Pili, ni ili uweze kutumia Maandiko kuwasaidia Wakristo walio wachanga kiroho kushinda wale wanaoshindana na ukweli wa Mungu
Wakorintho (sehemu ya pili aliyokwenda kufanya huduma) walikuwa na uchanga wa imani, ndio maana Paulo alisema habari ya kutengana kwao kwamba mmoja ni wa Apolo na mwingine ni wa Paulo (1Kor. 3:1-4)
Tit. 1:10 “Kwa maana kuna wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, wadanganyaji, na hasa wale wa tohara, ambao yapasa wazibwe vinywa vyao.”
JINSI YA KUFUNDISHWA KWA USAHIHI NJIA YA BWANA ILI UWE HODARI KATIKA MAANDIKO
Kwanza, ruhusu Roho Mtakatifu aimshe roho yako.
Stefano, mfia imani wa kwanza alishinda kwa hekima aliyopewa na Roho Mtakatifu
Mdo. 6:8-9
Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano, lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.
Yn.1426 Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
1Kor.2:13 “ Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni.”
Pili, kubali kuongezewa elimu na watu wengine
Watu wa kwanza waliokufundisha wokovu.
Apolo alifika Efeso, akiwa tayari amefundishwa njia ya Bwana (25)
Elimu hii ni ya watoto wachanga; ni maziwa; ni mafundisho ya awali.
Watu unaokutana nao katika huduma
Apolo alikutana na Prisila na Akila, nao wakamfundisha njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.
Efe. 4:11-12 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;”
Tatu, ili kushinda kabisa kabisa, tumia maandiko kuonyesha kuwa YESU NI KRISTO
----------------------
Kesheni, simameni imara katika Imani, fanyeni kiume, mkawe hodari.
Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.