UTANGULIZI
Historia
yake
Paulo ni mwalimu, mtume,
mwinjilisti na Myahudi ambaye jina lake la kwanza, la Kiyahudi
lilikua Sauli,
ambaye Bwana Yesu alimfanya chombo kiteule chake, ili alichukue
Jina lake mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Alizaliwa
Tarso, mji wa Kilikia, na kupelekwa Yerusalemu, akafundishwa Torati
kwa usahihi miguuni pa Gamalieli, ambaye ni Farisayo aliyekua maarufu
sana wakati huo (Mdo
22:3) Alikua na
ujuzi wa ufundi wa kutengeneza na kushona mahema (Mdo
18:3). Jina Paulo,
ni jina la Kirumi (Latin. ‘Paullus’)
ambalo lilikua jina la mbadala kwa sababu alikua na uraia wa Kirumi
na Kiyahudi, na ndilo lilimsaidia sana katika kueneza Injili katika
miji aliyokua akieneza Injili kwasababu ilitawaliwa na Warumi (Mdo
13:9).
Mateso
kwa Kanisa
Paulo aliliharibu, kulitesa na
kuliudhi kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na
wanawake na kuwatupa gerezani, akiwafunga, hata kwenda kwa Kuhani
Mkuu na wazee wa baraza na kupokea barua na kupita miji kwa miji
ili awalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili
waadhibiwe (Mdo 8:3;
Gal 1:11).
Alishiriki katika kifo cha mfia dini, Stefano naye ‘aona vema kwa
kuuwawa kwake’ kwani ndiye aliyeshika nguo za wale waliomwua
Stefano (Mdo 7:58;
22:20).
Kuongoka
Alitokewa na Bwana Yesu akiwa
anaelekea mji wa Dameski (Mdo
9:1-8) na kupewa
mafunuo (Gal
1:11-12) kwa ajili
ya kufanya kazi ya Bwana, akatiwa upofu, akakaa siku tatu bila kula
wala kunywa, kisha akawekewa mikono na Anania na kutolewa upofu,
kisha kubatizwa. Akaelekea Arabuni, kisha akarudi Dameski na kukaa
siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi, akihubiri Injili (Mdo
9:19; Gal 1:17).
Mchango
wa Mt. Paulo katika Kanisa la Kwanza.
Mwalimu
wa Neno la Mungu.
Paulo, kabla ya kutengwa na Roho
Mtakatifu kuwa mtume wa mataifa, alikua mmoja kati ya walimu na
manabii waliokuwapo katika Kanisa la Antiokia (Mdo
13:1); kwakuwa
alikua amefundishwa Torati na Rabi Gamalieli, basi alikuwa msaada
katika kufafanua maandiko na kuyaoanisha na Injili katika Kanisa la
Kwanza.
Mtume Paulo alikua na desturi ya
kuingia katika masinagogi ya Kiyahudi, katika kila mji alipokwenda
kuhubiri, hivyo ilimpasa ajue vizuri torati na kujua kuifafanua kwa
wale ambao ni Wayahudi, na hata wakati mwingine kwa Wayunani. Hii
inadhihirishwa sana alipokuwa mji wa Thesalonike, kwani aliingia na
“akahojiana
nao kwa maneno ya maandiko
sabato tatu, akiyafunua
na kuwaeleza ya
kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya
kwamba, Yesu huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo.”(Mdo
17:2-3).
Injili
kwa Mataifa
Paulo alipokuwa Yerusalemu,
akisali ndani ya Hekalu, Bwana Yesu alimtokea, akamwagiza akahubiri
kwa Mataifa (Mdo
22:18-21), pia
akiwa Antiokia pamoja na wanafunzi wengine, wakifunga na kuomba,
“Roho Mtakatifu
akasema, Nitengeeni
Barnaba na Sauli kwa kazi
ile niliyowaitia.”(Mdo 13:2b).
Kwani “(ali)kabidhiwa
injili ya
wasiotahiriwa,
kama vile Petro ya waliotahiriwa”(Gal
2:7).
Paulo, kwa ujasiri na msaada wa
nguvu za Roho Mtakatifu alihubiri katika miji mingi ya Asia ndogo
pamoja na Ulaya akishirikiana na Barnaba, Sila, Timotheo, Tito, Akila
na Prisila na wengine. Alipita katika miji ya Kipro (Salami na Pafo);
Pamfilia (Perge); Pisidia (Antiokia); Likaonia (Listra, Derbe); Troa;
Makedonia (Filipi); Thesalonike; Korintho; Ugiriki (Athene); Efeso;
Rumi n.k. (Mdo
13-21)
Kuanzisha
Makanisa mapya.
Paulo alifanya safari tatu za
kiuinjilisti na katika safari hizi aliweza kuanzisha makanisa katika
kila mji alioupita. Katika miji yote iliyotajwa hapo juu, alihubiri
Injili kwa ushujaa, kwa “ishara
na maajabu
ambayo Mungu aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa.”
(Mdo 15:12).
Katika kuhubiri kwake, “wengine
walikaidi,
wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi,
akaondoka akawaacha,
akawatenga
wanafunzi…”(Mdo:19:9).
Hivyo kwa waliokataa aliwaacha, na kuwatenga wanafunzi, na hao ndio
waliokuwa mwanzo wa makanisa
katika miji mbalimbali.
Ashiriki
Baraza la Kwanza la Yerusalemu
Baada ya Wayahudi kutoka
Yerusalemu kuwafundisha Wakristo wa mataifa ya kwamba, wasipotahiriwa
kama desturi ya Musa hawawezi kuokoka (Mdo
15:1), Paulo
na Barnaba walilazimika kwenda Yerusalemu, wakisafirishwa na kanisa,
ili kujadili mjadala huo. Kuhusu jambo hilo, kwa hekima ya Petro,
Paulo, Barnaba na Yakobo, lilitatuliwa na kutolewa suluhu na maamuzi
kwa moyo mmoja. (Mdo
15:1ff)
Kupitia mtaguso uliotolewa na
baraza hili (Mdo
15:23-29),
ndipo thelojia ya
‘(tu)meokolewa kwa
neema, kwa njia
ya imani;
ambayo hiyo haikutokana na nafsi ze(tu), ni kipawa cha Mungu;wala
si kwa matendo,
mtu awaye yote asije akajisifu.” (Efe
2:8-9;
Gal 2:16)
ilipoonyesha uimara
wake kama msingi mkuu wa Kanisa la Kikristo. Tatizo liloibuliwa na
Wayahudi lilikua na hatari ya kulitenganisha kanisa na bila shuhuda
za jinsi Mungu alivyotenda kazi kwa watu wa Mataifa kupitia Paulo na
Barnaba, pengine kanisa lingegawanyika.
Kuimarisha
Makanisa na kuteua Waangalizi (Maaskofu)
Baada ya kuanzisha na kuwatenga
wanafunzi katika miji aliyohubiri, Paulo na Barnaba, walirudi katika
miji ile,
“wakifanya
imara roho za
wanafunzi na kuwaonya
wakae katika ile Imani
…” (Mdo
15:22).
Paulo akishirikiana na Barnaba,
“waliwachagulia
wazee katika
kila kanisa, na
kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana
waliyemwamini” (Mdo
14:23). Moja
wa viongozi hawa walikua Timotheo, Tito pamoja na Akila na Prisila.
Hawa wote aliwaasa watunze nafsi zao, na kuwalisha kundi lote
lililoko chini yao, . (Mdo
20:28).
Barua
kwa Makanisa na kwa Wachungaji
Nyaraka alizoziandika Mtume Paulo
kwa makanisa ya Rumi, Galatia, Thesalonike n.k pamoja na kwa
wachungaji (Timotheo na Tito), ni hazina kubwa sana ambayo Roho
Mtakatifu, kwa kupitia Paulo, aliziacha kwa ajili ya kukuza uelewa na
theolojia yetu kuhusu Injili na Mungu kwa ujumla. Paulo aliandika
nyaraka takribani kumi na tatu (13), zilizoweza kuhifadhiwa hata sasa
na kuwekwa katika Biblia.
Roho Mtakatifu alimtumia Paulo
kusema na kanisa na kudhihirisha kweli halisi kwakuwa nyaraka hizi ni
Neno la Mungu, nazo zikawa funguo za kuonyesha ukweli kuhusu Kristo
kwa mataifa. Zilionyesha ukomavu wa Paulo katika imani yake, na hivyo
kuwa kielelezo kizuri kwa Kanisa la Kwanza na hata kwa vizazi vyote
vilivyofuata, kwani nyaraka hizi ni wazi ziliandikwa kabla ya Injili
kuandikwa, na kusomwa katika makanisa ya kipindi hicho.
Mambo
ya kujifunza kutokana na maisha na utumishi wa Mt. Paulo.
Mwinjilisti wa karne hii ya
ishirini na moja, anayo mengi sana ya kujifunza kutokana na maisha na
utumishi wa Mt. Paulo. Baada ya kujifunza kupitia maagizo ya Bwana
Yesu Kristo, mfano pekee wa kuiga na wa kielelezo wa namna ya
kuyaishi maisha yaongozwayo na roho, haswa kwa mtu ambaye hakuwa na
Uungu kama Yesu, ni maisha ya Mtume Paulo. Naye asema, ‘mnifuate
mimi kama mimi nilivyomfuata Kristo’ (1 Kor 11:1). Yafuatayo
ni mambo ya msingi ya kujifunza;
Neema
ya Mungu ni ya kipekee.
Ingawa Paulo (Sauli) alilitesa na
kuliudhi kanisa sana hapo mwanzo, neema ya Mungu ilimwinukia na
kumbadilisha toka chombo cha uharibifu, na kuwa chombo cha utakatifu.
Nguvu hii ya Mungu ndiyo neema yake, ambapo ilimstahilisha pasipo
yeye mwenyewe kustahili.
Hili likawa funzo na mkazo wake
mkubwa sana katika Injili na mahubiri yake, ikionyeshwa wazi katika
nyaraka zake kwa Warumi na Wagalatia, nayo kumvuta kusema, “ Kwa
maana mmeokolewa
kwa neema, kwa
njia ya imani; ambayo hiyo
haikutokana na nafsi zenu,
ni kipawa cha Mungu; wala
si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.(Efe
2:8-9). Hivyo
tutambue kwamba hata sasa Mungu anaweza kuwaokoa watu hata
wanaolitesa au ni wapinzani wa Kanisa, hata wale ambao ni waovu
wakubwa ambao hawadhaniwi kwamba waweza kuokoka, mfano wachawi, wezi,
wauwaji na hata waganga wa kienyeji.
Kufunga
na kuomba: nyenzo muhimu kuliko zote katika kanisa na utumishi.
Baada ya Sauli kutokewa na Bwana
Yesu na kupewa maono makubwa, alikwenda Dameski na alifunga bila kula
wala kunywa (Mdo
9:9) Hii ilikuwa
ili kumtayarisha kwa ajili ya huduma yake ya kufanya utume kwa
mataifa. Nasi kama tukitaka huduma yetu iwe na nguvu za Mungu, ni
vyema kufunga na kusali.
Kabla ya Roho Mtakatifu kumtenga
Paulo na Barnaba, mitume walikuwa wanafunga na kuomba (Mdo
13:2-3). Hii
ilisaidia katika kuachilia Roho Mtakatifu awe nyenzo kuu katika
kukuza Kanisa lake. Nasi tunapotaka Mungu afanye huduma kubwa naya
kipekee katika Kanisa la sasa, ni vyema tufunge na kusali.
Kabla ya kuwawekea mikono wazee
na waangalizi wa makanisa ya Listra, Derbe na Antiokia ya Pisidia,
Paulo na Barnaba walifunga na kuomba (Mdo
14:23. Hii
ilisaidia kuhakikisha kwamba viongozi waliochaguliwa, hawakua kwa
hekima na mtazamo wa wanadamu bali walitegemea Roho ndie awasimike.
Hata sasa ni vyema kufunga na kuomba kama twataka kusimika kiongozi
katika Kanisa, ili Roho Mtakatifu afanye kazi hiyo.
Paulo alisisitiza katika barua
zake kwamba alifunga na kuomba sana ili kupata nguvu ya kuendelea
kuhubiri injili.
Kuwekewa mikono au kusimikwa
– Kutengwa kwa ajili ya kazi ya Injili.
Baada ya Roho Mtakatifu kuwatenga
Paulo na Barnaba, mitume, “wakaweka
mikono yao juu yao,
wakawaacha waende zao.” (Mdo
13:3). Hii
ilionyesha kupokea baraka zote kutoka kwa viongozi wa juu ili kufanya
huduma.
Baada ya kuanzisha makanisa huko
Galatia “na
walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja
na kufunga, wakawaweka
katika mikono
ya Bwana waliyemwamini.”(Mdo
14:23). Hivyo nao
viongozi walioteuliwa na Paulo na Barnaba walisimikwa na kuwekewa
mikono.
Kusimikwa huku na kuwekewa mikono
humaanisha, hao waliotengwa kwa ajili ya huduma, wamepokea baraka na
neema zote kutoka kwa Mungu, kupitia viongozi waliopo. Hata sasa ni
vyema kwa mtumishi wa Mungu, kupitia hivyo na sio kama manabii wa
uongo wanaoibuka kila siku na kuwalaghai watu.
Mafunzo
na mafunuo ya KWELI hutoka kwa Yesu Kristo, sio wanadamu.
Paulo aliwajulisha Wagalatia
kwamba, “injili hiyo
niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna
ya kibinadamu. Kwa
kuwa sikuipokea
kwa mwanadamu
wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo
wa Yesu Kristo.(Gal
1:11-12). Japo
Paulo aliijua Torati sana na kufanya bidii, elimu na bidii yake
haikuweza kumleta katika Injili, bali Roho wa Mungu ndiye aliyempa.
Hakuna mwanadamu awezaye kwa
maneno yake kutuvuta kwa Mungu, bali Yesu asema waziwazi, “hakuna
mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.” (Yn
6:65)
Ujasiri
wa kuhubiri Injili
Mtume Paulo ni mfano wa kuigwa
kabisa kwa namna alivyokuwa jasiri katika kuhubiri Neno la Mungu kwa
mataifa. Alinena kwa ujasiri katika masinagogi ya Wayahudi, katika
kila mji alioutembelea, mbele ya makadhi na viongozi wa miji, mbele
ya askari wa Kirumi, Liwali wa Kirumi, Festo na hata mbele ya Mfalme
Agripa.
Hata mtumishi wa leo, yampasa
kuwa jasiri katika kuhubiri hata kama ni mbele ya watu wakubwa wa
kiserikali bila kuogopa cheo cha mtu wala nafasi aliyonayo; kwani
Bwana alisema, “kila
mtu atakayenikiri
mbele ya watu,
nami nitamkiri
mbele za Baba
yangu aliye mbinguni.” (Mt
10:32)
Imetupasa
kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.
Huu ndio ujumbe aliowapa kwa
maonyo na kuwaimarisha Wakristo waliokuwa katika makanisa ya Galatia,
baada ya yeye pamoja na Barnaba kupitia katika “taabu
na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika
kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi.” (2
Kor 11:27)
Mtumishi wa kipindi hiki lazima
ayakumbuke maneno ya Bwana kwamba, “Ulimwenguni
mnayo dhiki;
lakini jipeni
moyo; mimi
nimeushinda ulimwengu.”
(Yn
16:33b). Tusiwe
kama mbegu iliyopandwa kwenye miamba, ambapo dhiki ikitokea juu ya
Neno la Mungu, huliacha; bali tuwe kama Paulo, udongo mzuri ambapo
mbegu ilipopandwa ilikua na kuzaa matunda mengi.
Kufundisha, kulea na
kuimarisha wanafunzunzi wachanga katika imani.
Baada ya kuanzisha makanisa
katika miji yote, Paulo alimwambia Barnaba, “turejee
sasa tukawaangalie hao ndugu
katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani.”
(Mdo 15:36b).
Paulo aliwathamini
waongofu wapya katika Kristo, na hii pia hushuhudiwa kwa nyaraka zake
kumi na tatu, ambazo humo huonyesha kujali, kufundisha, kuonya na
mwendelezo wake wa kuwakuza kiroho wale aliotaabika kwa ajili yao.
Mtumishi hasa mwinjilisti,
yampasa kurudi na kuwalea kiroho wanafunzi wale ambao aliwapata
katika Injili kwa njia ya semina, warsha na mafundisho mbalimbali.
Hii imepungua sana kwani siku hizi tunaona mikutano ya Injili lakini
semina chache pamoja na ufuatiliaji hafifu sana kwa wale walioongoka
baada ya mikutano ya Injili.
Kulijua
Neno la Mungu vizuri na kutambua walengwa wasikiao Injili.
Paulo alijua sana Agano la Kale,
na hii yadhihirishwa kwa namna kila alipoingia katika masinagogi na
kunukuu mara nyingi na kwa usahihi Maandiko matakatifu. Hivyo
mtumishi lazima kuyasoma, kuyatafakari na hata kuyakariri maandiko
ili yaweze kumsadia kuhubiri kwa usahihi na umakini bila kuyumbishwa.
Akiwa kwa Wayahudi, Paulo
alitumia vizuri Torati na Manabii kuwaelezea kuhusu Yesu, lakini
alipokuwa na Wayunani, mjini Athene, alibadilika na kutumia mazingira
yao, na taratibu zao ili kufikisha Injili – kupitia ‘Mungu
Asiyejulikana’ (Mdo
17:23). Pia
alipokuwa katika miji ya Likaonia, baada ya watu kudhani yeye ni
mungu, alifafanua kuhusu Mungu kupitia ‘mafunuo
ya kawaida’ au
‘general revelation’
kama msingi wa kuhubiri Injili.
HITIMISHO
Yapo mengi sana ya kujifunza
kupitia utumishi na maisha ya Paulo ambayo hayawezi elezewa hapa
yote, lakini mausia yafuatayo yatosha kujua juhudi zake katika
kumtumikia Mungu;
“Lakini mambo yale
yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara
kwa ajili ya Kristo.
Naam,
zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa
ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu,
Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote
nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane
katika yeye,
nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile
ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa
Mungu, kwa imani; ili nimjue
yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake,
nikifananishwa na kufa kwake; ili
nipate kwa njia yo yote kuifikia
kiyama ya wafu. Si
kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali
nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake
nimeshikwa na Kristo Yesu.”
Flp 3:7-12
AMEN
_________________
Vitabu Rejea:
Swahili Union Version,
Biblia Takatifu,
1997
Don Fleming,
Kamusi ya Biblia,
2016
London, The Inter-Varsity
Fellowship, The
New Bible Commentary,
1958
www.wikipedia.com,
Free Wikipedia,
2019