Tuesday, March 17, 2026

MADHARA YA KULEGEA

 


Kulegea Katika Majukumu - Pastor Obed Joseph Katunzi

Utangulizi

Kila mwanadamu aliye hai duniani ameumbwa kwa kusudi maalum. MUNGU hakumuumba mtu yeyote kwa bahati mbaya, wala hakuna mtu aliye hapa duniani kwa makosa. Kila mtu anao wajibu aliokabidhiwa na Muumba wake, na majukumu hayo yanaweza kujidhihirisha kwa njia tofauti kulingana na nafasi, wito, au mazingira ya maisha ya mtu huyo.

Majukumu haya yanaweza kuwa:

Ya kifamilia (kama mzazi, mtoto, mume, au mke)

Ya kikazi (kama mfanyakazi, meneja, mkulima, mjasiriamali, n.k.)

Ya huduma ya kiroho (kama mhubiri, mwimbaji, mwinjilisti, mshauri, au muombezi)

Ya kijamii (kama kiongozi wa jamii, msaidizi wa wengine, au raia mwema)

Ni muhimu kufahamu kwamba majukumu haya si kwamba yapo tu, bali ni sehemu ya kusudi la MUNGU juu ya maisha ya mtu. MUNGU alipomuumba mwanadamu katika kitabu cha:

Mwanzo 1:28

"MUNGU akawabarikia, MUNGU akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi."

MUNGU alimpa mwanadamu jukumu la kutawala, kuzaa, kujaza dunia na kuitiisha. Hii inaonyesha kwamba majukumu ni sehemu ya agizo la KIMUNGU tangu mwanzo wa uumbaji.

Maisha ya mtu hayawezi kuwa na maana kamili bila kutambua na kutekeleza majukumu yake. Mafanikio ya mtu kiuchumi, kiroho, kihisia au kijamii yanategemea kwa kiwango kikubwa namna anavyotimiza wajibu wake kwa uaminifu. Hata hatima ya mtu — kile atakachokuwa au kufanikisha mwisho wa maisha yake — imo ndani ya uaminifu wake katika kutekeleza majukumu hayo.

+ + +

Kulegea Katika Majukumu

Hata hivyo, changamoto kubwa inayowakumba wengi ni kulegea katika majukumu yao. Ulegevu ni hali ya kupungua kwa bidii, uzito au uthubutu wa kutekeleza majukumu kama ilivyokusudiwa. Mtu anaweza kuwa anaonekana anafanya jambo, lakini hana moto wa ndani, hana uaminifu, au amepoteza mwelekeo.

Yeremia 6:24

"Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na utungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake."

Katika aya hii, tunaona kwamba ulegevu wa mikono si tu wa kimwili, bali ni matokeo ya hali ya ndani ya kiroho na kiakili. Wanadamu wanapopokea habari za hofu, mashambulizi, au hatari, hali yao ya ndani hubadilika. Moyo unayeyuka, na matokeo yake ni:

Kudhoofika kwa juhudi

Kupungua kwa ari ya kufanya kazi

Kupotea kwa tumaini

Kujitoa katika wajibu

Kuingia katika dhiki ya nafsi na mwili

Hali hii inafananishwa na utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa — hali ya uchungu mkubwa, kutoweza kuendelea mbele wala kurudi nyuma. Maumivu makali ambayo mtu hana budi kuyakabili hadi mwisho. Hii ni picha ya uzito wa madhara ya ulegevu: kwamba mtu anapoacha majukumu yake, ni kama mwanamke aliyekaribia kuzaa lakini hana msaada au nguvu ya kumaliza safari yake ya uchungu.

+ + +

Ulegevu Kama Roho

Zaidi ya kuwa hali ya kawaida, ulegevu ni roho ya kishetani inayotumwa ili kuzuia mafanikio na kuyumbisha watu kutoka katika kusudi la MUNGU. Shetani huingiza roho hii ili:

Mtu apoteze ari ya kufanya kazi

Aishi maisha ya uvivu, kuahirisha, na kujitetea

Aache huduma au wajibu wa kiroho

Asitimize ndoto au wito wake

Ahisi hana maana wala mchango katika jamii

Hili ni jambo la hatari sana. Watu wengi wanashindwa si kwa sababu hawana vipawa au nafasi, bali wameshindwa kupigana dhidi ya roho ya ulegevu iliyoingia ndani yao.

+ + +

Uhusiano wa Ulegevu na Uharibifu

Pale ambapo mtu analegea au kupuuza majukumu yake:

Kazi yake inaharibika

Uaminifu wake unapotea

Wale waliomtegemea wanaumia

Kusudi la MUNGU juu yake linachelewa au kuvurugika

Hii ni sawa na askari aliye mstari wa mbele kwenye vita lakini akaamua kupumzika katikati ya mapigano. Atahatarisha maisha yake na ya wengine. Vivyo hivyo, mtu anapoacha majukumu yake, anaacha "safu ya mapambano", na madhara yake huwa makubwa sana — kiroho, kihisia, kifamilia, na hata kimwili.

Kwa hiyo, kabla hatujaanza kuelezea aina za ulegevu na madhara yake, ni muhimu kila mmoja ajitazame mwenyewe kwa uaminifu:

Je, unajua majukumu yako yote kama mzazi, mfanyakazi, Mkristo au kiongozi?

Je, unayatendea kwa uzito, bidii na heshima inayostahili?

Je, umegundua kwamba kuna sehemu ya maisha yako umeshindwa kusimama imara?

Je, unahisi kuna roho ya uvivu au kukata tamaa inayozuia maendeleo yako?

Ikiwa majibu yako yanakuelekeza kwenye ulegevu, basi somo hili ni kwa ajili yako. Ni muda wa kurudi katika nafasi yako na kusema kama Nehemia:

Nehemia 6:3

"Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka."

MUNGU amekupa kazi kubwa sana — iwe ni katika familia, huduma, kazi au maisha yako binafsi. Usikubali roho ya ulegevu ikukatishe tamaa. Katika somo hili, tutaona sababu, madhara, na jinsi ya kushinda ulegevu katika kila eneo la maisha yako.

+ + +

Maana ya Kulegea Katika Majukumu

Kulegea ni hali ya kupungukiwa na nguvu, bidii, uthubutu na uaminifu katika kutimiza majukumu. Ni hali ya kupoteza moto wa ndani uliomuwezesha mtu kuwa na shauku ya kutimiza kile alichoitwa au kupewa afanye.

Isaya 13:7–8

"Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka. Nao watafadhaika; watashikwa na utungu na maumivu; watakuwa na utungu kama mwanamke aliye karibu na kuzaa."

Hii inatuonyesha kwamba kulegea kunaweza kuwa ni matokeo ya woga, habari za kutisha, mashambulizi ya kiroho au kukosa mtazamo sahihi wa kazi au huduma.

+ + +

Sababu za Ulegevu

1. Taarifa na Habari za Hofu

Yeremia 6:24

"Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na utungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake."

Katika maandiko haya, tunaona kwamba kusikia tu habari kunaweza kumvunja mtu nguvu kabisa. Watu wa Israeli waliposikia habari za adui anayewakaribia, hawakupigana kwanza, wala hawakupigwa — walilegea tu kwa kusikia. Hii inaonyesha kwamba habari au taarifa ni silaha kubwa kiroho.

Taarifa mbaya zinaweza kuathiri:

Mawazo yako — zinaingiza hofu, mashaka na sintofahamu.

Kutokuwa na Imani — kunaondoa tumaini na ujasiri wa ndani.

Mtazamo wako — unakosa kuangalia mambo kwa jicho la MUNGU na kuanza kuona kwa jicho la mwili.

Uamuzi wako — mtu anaweza kuahirisha au kuacha jambo muhimu kwa sababu tu ya taarifa.

Mfano wa Maisha Halisi:

Mfanyakazi anapambiwa na wenzake kazini kuwa "bosi hakupendi", anaweza kuanza kulegea kwenye juhudi zake, hata kama hakika hiyo haipo.

Mhubiri anaposikia watu wakimsema vibaya, anaweza kukata tamaa na kuacha huduma.

Taarifa za uongo au uzushi zinaweza kuwa:

Maneno ya wivu

Majungu na umbeya

Tafsiri mbaya za hali fulani

Uongo wa kishetani unaoenezwa ili kuua bidii ya mtu

Jihadhari sana na taarifa unazopokea, na chunguza vyanzo vyake kabla hujafanya uamuzi au kujiruhusu kuathiriwa kiakili na kiroho.

2. Mioyo Inayoyeyuka kwa Hofu

Isaya 13:7

"Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka."

Mioyo inayoyeyuka ni ishara ya hali ya ndani ya kiroho inayovunjika kutokana na hofu, mashaka, au maumivu. Hofu ni mtego wa kiroho unaozuia watu kutekeleza wajibu wao.

Hofu inaleta nini?

Kutokujiamini — mtu haoni thamani wala uwezo ndani yake.

Uoga wa kushindwa — mtu anahisi atashindwa kabla hajaanza.

Kulalamika — mtu anaanza kulaumu mazingira badala ya kutenda.

Kumbuka: Hofu haibebi ukweli wowote halisi, bali ni uvuli wa uongo unaotengenezwa na shetani ili kukufanya usisonge mbele.

Hesabu 13:32–33

32 Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno.

33 Kisha, huko tuliwaona wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.

Hofu hiyo iliwaingiza katika ulegevu — wakaacha kusonga mbele katika ahadi ya MUNGU. MUNGU aliwakasirikia sana hadi wakapoteza urithi wao.

Hofu ni mbolea ya ulegevu — unapoiruhusu ndani yako, unashindwa hata kuanza kutekeleza wajibu wako.

3. Mashambulizi ya Adui (Shetani)

Nehemia 6:2–3

2 Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Walakini wakakusudia kunifanyia mabaya.

3 Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?

Shetani huwa hatulii — kila anapoona mtu yuko katika mstari wa kutimiza kusudi lake, anaanza kupanga mipango ya kumuondoa kwenye mstari huo. Anatumia njia kama:

Hila za kisiasa au kijamii

Maneno ya kukatisha tamaa

Migogoro ya ghafla

Mapingamizi ya kifamilia au kifedha

Nehemia alikuwa na kazi kubwa ya kujenga ukuta wa Yerusalemu. Lakini adui zake walikusudia kumsimamisha — si kwa vita ya moja kwa moja, bali kwa kutumia mialiko ya nje ya kazi — mbinu ya kuvuruga mwelekeo wake.

Kanuni muhimu: Mtu anapopoteza mtazamo wa kile anachokifanya, au kusudi la MUNGU juu ya maisha yake, atakumbwa na ulegevu. Ukishavurugwa mwelekeo, haichukui muda kuanza kulegea mikono na moyo.

Suluhisho ni kuwa na maono thabiti, maombi ya kufunua hila za adui, na roho ya utambuzi kama Nehemia.

4. Manabii wa Uongo

Nehemia 6:12

"Nikatambua, na tazama, siye MUNGU aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; nao Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri."

Shetani ni mjanja — anajua kwamba si kila mtu anaweza kusikiliza watu wa kawaida, hivyo anatumia watu wa dini, wanaoonekana wa kiroho, wenye "karama", lakini wamepotoka mwelekeo wa MUNGU. Nehemia alifuatwa na mtu aliyeonekana kama nabii, ambaye alimtaka aingie hekaluni kwa hofu ya kuuawa. Lakini Nehemia alitambua rohoni mwake kwamba hilo halikutoka kwa MUNGU.

Hatari ya Manabii wa Uongo:

Hutoa "maono" ya hofu na si ya matumaini.

Wanakuvuruga mwelekeo badala ya kukuimarisha.

Wanakuambia uache kazi, huduma, au nafasi, ilhali MUNGU hajasema hivyo.

Wanakutengenezea hofu na mashaka kwa watu wa karibu — kaka, dada, mama au baba na ndugu wa karibu wanaweza kukutengenezea vita vya mwili kwa kukuambia kuwa hawa ni wachawi, mkaingia kugombana mwilini. Wanaweza kukwambia ni wachawi ili usiweze kuwasaidia, na unaingia katika hofu na kutokuwasaidia — na moja kwa moja unaingia katika dhambi.

1 Timotheo 5:8

"Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini."

Waefeso 6:12

"Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."

Njia ya Kujilinda

Pima roho (1 Yohana 4:1) — "Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani."

Linganisha unabii na Neno la MUNGU.

Omba MUNGU akupe utambuzi wa kiroho.

Mtu asipokuwa makini, anaweza kuacha kabisa kusudi lake kwa sababu tu ya "maono" au "ndoto" zisizotoka kwa MUNGU.

5. Ukosefu wa Maarifa ya Kiroho

Hosea 4:6

"Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa."

Mara nyingi mtu anapoonekana mlegevu au asiyewajibika, si kwa sababu ni mvivu, bali hana maarifa ya kiroho kuhusu ukubwa wa majukumu aliyonayo.

Ukosefu wa maarifa huathiri nini?

Utambulisho wako — mtu hajui yeye ni nani katika Kristo.

Majukumu yako — mtu hajui kwa nini yuko kwenye ndoa, huduma au kazi.

Hatima yako — mtu hajui wapi anaelekea, na hivyo hana sababu ya kujitahidi.

Mfano: Mtu akipewa nafasi ya kuwa kiongozi kanisani lakini hajui umuhimu wa wito huo, atafanya kazi hiyo kwa ulegevu, mazoea, na bila bidii yoyote.

Kujua kusudi la MUNGU juu ya maisha yako kunakuwezesha kupigana kulitimiza.

Sababu hizi tano ni baadhi ya silaha kuu anazotumia shetani kuleta ulegevu:

Habari za hofu — zinavunja moyo.

Mioyo inayoyeyuka — inaua ujasiri wa ndani.

Mashambulizi ya adui — yanapoteza mwelekeo.

Manabii wa uongo — wanapotosha watu kutoka kwenye kusudi.

Ukosefu wa maarifa — unafanya watu wachukulie majukumu kijuu juu.

Mtu anayezielewa na kujikinga dhidi ya hizi sababu ataimarika kiroho, atajua kutunza nafasi yake, na atashinda vita ya ulegevu katika maisha yake.

+ + +

Madhara ya Kulegea Katika Majukumu

1. Dhiki na Machungu

Mikono inapolegea, dhiki huingia.

Yeremia 6:24

"Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na utungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake."

Ulegevu huleta uchungu wa nafsi.

2. Baraka Kufungwa

Yeremia 48:10

"Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu; na alaaniwe auzuiaye upanga wake usimwage damu."

Ulegevu katika kazi ya MUNGU huleta laana badala ya baraka. Mtu anaweza kujikuta anafanya kazi lakini hana matokeo kwa sababu ya mkono mlegevu.

3. Kujitoa kwenye Kusudi la MUNGU

Nehemia alifahamu kwamba alikuwa anafanya kazi kubwa. Kama asingekataa mwito wa Sanbalati, angeacha kazi ya MUNGU isifanyike.

Nehemia 6:3

"Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?"

4. Kupoteza Nguvu za Kiroho

Ulegevu huondoa nguvu za kiroho. Hata sala na maombi huonekana kama mzigo. Mtu hachukui tena muda kusali, kusoma Neno au kufanya kazi ya Bwana kwa bidii.

5. Kupoteza Uongozi wa Kiungu

Msumari uliokazwa ukiwa imara, unaweza kubeba mzigo. Lakini ukilegea, kila kitu kinachoegemea juu yake huanguka.

Isaya 22:25

"Katika siku ile, asema Bwana wa majeshi, ule msumari uliokazwa katika mahali palipo imara utalegea; nao utakatwa na kuanguka chini, na ule mzigo uliokuwa juu yake utakatiliwa mbali; maana Bwana amesema haya."

Hii inamaanisha kwamba mtu anapolegea, hata wale waliomtegemea (familia, huduma, jamii) huathirika.

+ + +

Sehemu Ambazo Roho ya Ulegevu Hushambulia

1. Kazini

Roho ya ulegevu inapomshambulia mtu kazini, huonekana kwa njia mbalimbali:

Kuchelewa kazini mara kwa mara

Kutokamilisha kazi kwa wakati

Kutokuwa na ubunifu au hamasa kazini

Kuwalaumu wengine badala ya kuwajibika

Kufanya kazi kwa mazoea, bila ubora au moyo wa kujitoa

Mtu aliyelegea kazini hawezi kuwa baraka mahali pa kazi. Anapoteza fursa za kupandishwa cheo, kuaminiwa zaidi, au kupata baraka kutoka kwa MUNGU.

Mithali 18:9

"Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharabu."

Hii inaonyesha kwamba ulegevu kazini ni sawa na uharibifu. Ukifanya kazi kwa mkono mlegevu, unaharibu: biashara ya mtu mwingine, kipato chako mwenyewe, na imani ya wengine juu yako.

Hatari: Kupoteza kazi au mteja; kukosa mafanikio ya kiuchumi; kuvuruga ushuhuda kama Mkristo.

Suluhisho

Omba neema ya MUNGU kufanya kazi zako kama kwa Bwana:

"Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu." (Wakolosai 3:23)

Kuwa na ratiba na maadili ya kazi. Jifunze kujiongoza hata pasipo kusimamiwa.

2. Huduma ya MUNGU

Katika huduma, ulegevu huingia kwa njia kama: kuchelewa ibadani au kuacha kabisa kushiriki ibada, kupoteza ari ya kuomba au kusoma Neno, kutotii maagizo ya kiroho au kutokuwa tayari kusaidia, kukosa moyo wa kujitoa kwa kazi ya MUNGU.

Mtu aliyekumbwa na roho ya ulegevu kihuduma hufanya mambo ya MUNGU kwa kulazimishwa au kwa mazoea. Hii ni hatari sana kwa sababu huduma si kazi ya kawaida — ni agizo la MUNGU juu ya maisha yako.

Yeremia 48:10

"Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu; na alaaniwe auzuiaye upanga wake usimwage damu."

Ulegevu katika huduma ni laana, siyo tu uzembe. Mtu akiendelea kulegea katika huduma, anaweza:

Kupoteza upako na nafasi yake

Kuwa sababu ya kuanguka kwa wengine

Kuangamiza kizazi chake kwa kutotimiza kusudi la MUNGU

Dalili za ulegevu kiroho:

Maombi ya haraka haraka au ya kulala

Kujisahau katika huduma kwa visingizio vya kazi au familia

Kukwepa majukumu ya kiroho kama kutoa, kushuhudia, au kufundisha

Suluhisho

Kumbuka ni kwa neema ulivyookolewa — jitie moyo kumtumikia MUNGU.

Omba ROHO MTAKATIFU akupe bidii na ari mpya.

Jitahidi kuwa na ratiba ya maombi, Neno, na ibada.

3. Ndoa na Familia

Katika ndoa, roho ya ulegevu inaathiri kwa njia ya: kutokujali hisia za mwenzi wako, kupunguza mawasiliano ya kihemko au ya kiroho, kupuuzia malezi ya watoto, kutokuwa na juhudi ya kufanya ndoa iwe bora.

Wanandoa wengi wameachana si kwa sababu ya dhambi kubwa, bali kwa sababu ulegevu uliingia polepole. Walianza kwa kupunguza mazungumzo, kisha wakaacha kuomba pamoja, kisha kila mmoja akaanza kuishi kivyake.

1 Petro 3:7

"Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe."

Maisha ya ndoa yanahitaji ufahamu na bidii ya kiroho, kiakili na kihisia.

Madhara ya ulegevu katika ndoa:

Migogoro ya mara kwa mara

Kukosekana kwa amani ya nyumbani

Watoto kulelewa katika mazingira ya migogoro

Kukatisha ndoto na huduma za familia

Suluhisho

Rekebisha mawasiliano — ongea, sikiliza, samehe.

Weka ratiba ya maombi ya pamoja.

Fanya juhudi kulinda na kujenga uhusiano kila siku.

4. Afya

Roho ya ulegevu haishambulii tu mambo ya kiroho au ya kiuchumi — huathiri hata mwili wako. Ulegevu katika afya huonekana kwa:

Kutokula vyakula vya afya

Kutojishughulisha kimwili

Kutokunywa maji ya kutosha

Kupuuzia kupumzika au kulala vizuri

MUNGU anatupenda kiroho na kimwili. Mwili ni hekalu la ROHO MTAKATIFU:

1 Wakorintho 6:19

"Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la ROHO MTAKATIFU aliye ndani yenu, mliyepewa na MUNGU? Wala ninyi si mali yenu wenyewe."

Kuacha kujitunza kiafya ni njia ya kulikaribisha gonjwa na uchovu usio wa lazima.

Madhara ya ulegevu katika afya:

Magonjwa ya moyo, kisukari, uzito kupita kiasi

Kushindwa kuwa na nguvu za kiroho (kwa sababu ya uchovu wa mwili)

Kupoteza muda mwingi hospitalini au kutumia fedha nyingi kwa matibabu

Jinsi ya Kukabiliana

Jishughulishe kimwili angalau dakika 20, hata kwa kufanya mazoezi ya kutembea.

Kula kwa utaratibu na uzingatie lishe bora.

Omba neema ya kuwa na nidhamu ya maisha.

5. Maono Binafsi (Ndoto na Malengo ya Maisha)

Hili ni eneo nyeti sana. Watu wengi wamepata maono kutoka kwa MUNGU kuhusu huduma, biashara, kazi au elimu. Lakini baada ya muda, roho ya ulegevu huingia, na mtu: anaanza kukata tamaa, anaahirisha kila kitu, anaacha kujiendeleza, anapoteza matumaini kabisa.

Mithali 29:18

"Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria."

Ukikosa maono au ukayapuuza, utaishi bila nidhamu, bila juhudi, na mwisho bila matokeo. Roho ya ulegevu ni silaha ya shetani ya kuua maono ya mtu kabla hayajatimia.

Dalili za ulegevu kwenye maono:

Kutokuwa na ratiba au mpango wa maendeleo

Kusubiri "hali iwe sawa" kabla ya kuanza

Kusahau kabisa kile MUNGU alikuonyesha au kukusudia

Shughulikia Hivi

Andika tena maono yako na uyaombe kila siku:

"Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji." (Habakuki 2:2)

Tafuta watu wa kukuunga mkono au kukutia moyo.

Chukua hatua ndogo kila siku kuelekea lengo lako.

Roho ya ulegevu hushambulia kila eneo muhimu la maisha, ili kumvunja mtu nguvu kabla hajafikia kilele cha kusudi lake. Ukiiona sehemu yoyote kati ya hizi tano imeathirika: ujue roho ya ulegevu imeshaanza kufanya kazi, na ni lazima uchukue hatua haraka.

Zaburi 18:34

"Ananifundisha mikono yangu vita, Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba."

MUNGU anakupa nguvu mpya leo ya kuipiga roho ya ulegevu katika kila eneo la maisha yako.

+ + +

Suluhisho Dhidi ya Ulegevu

1. Tambua Nafasi Yako na Kazi Ulioitiwa

Kama Nehemia, tambua kwamba unafanya "kazi kubwa". Ukielewa kwamba unahusika katika mpango wa MUNGU, hutapoteza mwelekeo kwa urahisi.

2. Omba kwa Bidii

Zaburi 77:2

"Siku ya taabu yangu nalimtafuta Bwana; Mkono wangu ulinyoshwa usiku, haukulegea; Nafsi yangu ilikataa kufarijika."

Maombi huimarisha mikono iliyolegea. Lazima ujenge utamaduni wa maombi ya kila siku.

3. Pambana na Roho ya Ulegevu

Roho ya ulegevu ni pepo, na YESU aliifukuza kwa mamlaka.

Marko 7:35

"Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri."

BWANA YESU alitumia mamlaka yake kukata vifungo. Sisi pia tunayo mamlaka.

4. Kata Taarifa Mbaya

Epuka vyanzo vya taarifa zinazolegeza moyo wako. Watu wa uzushi, wenye maneno ya kukatisha tamaa, ni silaha ya adui. Linda moyo wako.

5. Omba kwa Ajili ya Moto Mpya

Moto wa kiroho unapowaka ndani yako, ulegevu haupati nafasi.

Zaburi 77:3

"Nilipotaka kumkumbuka MUNGU nalifadhaika; Nilipotaka kutafakari roho yangu ilizimia."

Usikubali roho ya ulegevu ikukatishe tamaa.

Simama imara. Fanya kazi kubwa uliyoitiwa. Hata nisiweze kushuka.

Mwandishi
Pastor Obed Joseph Katunzi

Ubatizo Sahihi ni Huu

Ubatizo Kibiblia Utangulizi Moja ya somo Muhimu sana kwa mkristo anayetarajia...