Thursday, March 26, 2026

Ubatizo Sahihi ni Huu

Ubatizo Kibiblia

Utangulizi

Moja ya somo Muhimu sana kwa mkristo anayetarajia kuingia mbinguni. Bila ubatizo wa kweli mtu hataweza kuingia katika ufalme wa MUNGU. Mtu asiyebatizwa katika ubatizo wa kweli hatambuliki katika kitabu cha uzima katika ufalme wa MUNGU.

Ubatizo ni Nini

Ubatizo kibiblia ni tendo takatifu lililoamriwa na MUNGU, linaloonyesha toba ya dhambi, kuokoka, na kuanza maisha mapya ndani ya KRISTO. Ni ishara ya nje inayoonyesha kile kilichotokea ndani ya moyo wa mtu.

Maana ya Ubatizo Kibiblia

Maana yake ya kwanza ni Kuzikwa na kufufuka pamoja na KRISTO, Biblia inasema;

Warumi 6:4

Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama KRISTO alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.

Hii ina maana kwamba unapobatizwa
  • Unazikwa dhambi zako za zamani
  • Unafufuka kuishi maisha mapya
  • Ishara ya toba ya kweli
  • Ubatizo unaambatana na kuacha dhambi
Matendo 2:38

Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha ROHO MTAKATIFU.

Hivyo ubatizo si kuoga tu, bali ni uamuzi wa kuacha maisha ya zamani.

Kuingia katika familia ya MUNGU. Ni ishara ya kuunganishwa na YESU KRISTO na kuwa sehemu ya mwili wake yaani kanisa.

Kufuata Mfano wa YESU KRISTO

YESU KRISTO mwenyewe alibatizwa. Hivyo kama sisi ni wanafunzi wake, na tunajifunza kwake, lazima na sisi tubatizwe. Maandiko yanasema,

Mathayo 3:13–17

13 Wakati huo YESU akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe.

14 Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?

15 YESU akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali.

16 Naye YESU alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona ROHO wa MUNGU akishuka kama hua, akija juu yake;

17 na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye,

Hivyo ubatizo ni ishara kwamba yeye anayefanya hivyo anamtii MUNGU kwa kufuata maelekezo yake. Maana Yesu alifanya hivyo kwa kutimiza na kufuata maelekezo kutoka kwa Baba.

Kubatizwa kwa Maji Mengi / Kuzamishwa

Neno "Ubatizo" linatokana na neno la Kigiriki BAPTIZO linalomaanisha "KUZAMISHA."

Hivyo ubatizo wa kibiblia unafanyika kwa kuzamishwa majini, si kunyunyiziwa. Hivyo tendo la ubatizo kwa usahihi linapaswa kufanyika kwa kuzamishwa ndani ya maji mengi.

Kwa maana imeandikwa

Yohana 3:5

YESU akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa ROHO, hawezi kuuingia ufalme wa MUNGU.

Na kule kuzamishwa kunamaana kubwa sana yaani kufa na kufufuka. Tunapozamishwa ni ishara ya kitendo cha kufa na tunapoibuka ni ishara ya kitendo cha kufufuka pamoja na KRISTO.

Warumi 6:4

Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama KRISTO alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.

Kwa hiyo ubatizo usio sahihi utawapeleka wengi katika jehanamu ya moto. Tutajifunza kuhusu ubatizo wa jina la Baba, mwana na ROHO MTAKATIFU ni sahihi au sio sahihi kulingana na maandiko

Kwa maana imeandikwa

Mathayo 28:19

Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la baba, na Mwana, na ROHO MTAKATIFU;

Katika somo hili tujifunze ubatizo wa kweli kwa jina la BWANA YESU kwa kuangalia vipengele hivi;

  1. SIRI ILIYO JIFICHA KATIKA BABA, MWANA, ROHO MTAKATIFU
  2. JINSI MITUME WALIVYOBATIZA UBATIZO WA JINA LA YESU

I: Siri Iliyo Jificha Katika Baba, Mwana, ROHO MTAKATIFU

TUANGALIE KUHUSU BABA

Kwa kusudi la kuelewa maana ya Baba, mwana na ROHO mtakatifu. Tutaenda kuchambua kwa undani ili tuelewe zaidi na Katika kipengele hiki tutaona nafasi ya baba katika familia. MUNGU amemuweka baba kuwa kichwa cha familia. Familia au ngazi ya familia inafananishwa na utawala wa MUNGU na MUNGU mwenyewe ndiye mwanzilishi wa familia. Tuangalie katika biblia tuone jinsi nafasi au ofisi ya Baba imeelezwa.

Mambo 4 Yanayomhusu Baba Ndani ya Familia Yake Katika Biblia

  1. Mtawala, kichwa au mfalme
  2. Mlinzi wa familia
  3. Mtoaji
  4. Mweka nidhamu

1. Baba: Mtawala, kichwa au mfalme

Baba Ameitwa kiungu kuwa nabii, kuhani, na mfalme katika nyumba yake, ili kuifundisha familia yake kutoka kwa Neno la MUNGU, kudumisha familia yake katika njia ya haki ya MUNGU, na kutawala familia yake kulingana na mapenzi ya MUNGU.

Habakuki 3:13

Ukatokea kwa ajili ya wokovu wa watu wako, Kwa ajili ya wokovu wa masihi wako; Ukakiponda kichwa cha nyumba ya waovu, Ukiuweka wazi msingi hata mwambani.

Hesabu 1:4–5

Tena mtu mume mmoja wa kila kabila atakuwa pamoja nanyi; kila mmoja aliye kichwa cha nyumba ya baba zake. Na majina ya hao waume watakaosimama pamoja nanyi ni haya; Wa Reubeni; Elisuri mwana wa Shedeuri.

Waefeso 5:22–24

Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii BWANA wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama KRISTO naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo KRISTO vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.

Hapa tunaona baba katika familia amepewa na fasi ya kuwa mtawala na kuwa kiongozi katika familia.

2. Baba: Mlinzi wa Familia

Akina baba wapo ili kuilinda familia, baba anapoacha kuilinda familia ndipo adui upata nafasi ya kuivamia familia. Tuone Mfano wa Mfalme wa Wafilisti Akishi Aliposhambulia Familia ya Daudi

1 Samweli 30:1–5

Ikawa, Daudi na watu wake walipokuwa wamefika Siklagi siku ya tatu, hao Waamaleki walikuwa wameshambulia Negebu, na Siklagi, nao wameupiga Siklagi, na kuuchoma moto; nao wamewachukua mateka wanawake waliokuwamo wakubwa kwa wadogo; hawakuwaua wo wote, ila wakawachukua, wakaenda zao. Basi Daudi na watu wake walipoufikilia mji, tazama, ulikuwa umechomwa moto; na wake zao, na watoto wao, waume kwa wake, wamechukuliwa mateka. Ndipo Daudi na watu waliokuwa pamoja naye wakainua sauti zao na kulia, hata walipokuwa hawana nguvu za kulia tena. Na hao wake wawili wa Daudi walikuwa wamechukuliwa mateka, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, aliyekuwa mkewe Nabali, wa Karmeli.

Hapa Daudi alikuwa mlinzi na alipewa jukumu la kuilinda nyumba yake dhidi ya mashambulizi kutoka kwa adui

3. Baba: Mtoaji wa Familia

Baba mara nyingi ukaa nafasi ya mtoaji wa familia. Kujishughulisha na kazi ili kuilea familia yake na kutoa mahitaji mbalimbali kama vile malazi, mavazi, chakula, elimu, na huduma za afya.

1 Timotheo 5:8

Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.

4. Baba: Muweka Nidhamu

Waebrania 12:7

Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; MUNGU awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?

Waefeso 6:4

Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya BWANA.

Kwa Hiyo Katika Ulezi, MUNGU Anasimama Katika Nafasi ya Baba, Mfalme, Mtawala. MUNGU ameonyesha Ubaba Wake kwetu kwa njia ya moja kwa moja kwa kuumba vitu vyote na kuanzisha mwanadamu, na kwa kuweka agano na uzao wake. MUNGU pia anaonyesha Ubaba Wake kwa njia ya upatanishi.

Isaya 63:15–16

tazama toka mbinguni, ukaone toka makao ya utukufu wako na fahari yako; uko wapi wivu wako, na uweza wako? shauku ya moyo wako, na huruma zako zimezuiliwa kwangu. Maana wewe ndiwe Baba yetu, ijapokuwa Ibrahimu hatujui, wala Israeli hatukiri; wewe, BWANA, ndiwe Baba yetu, mkombozi wetu tangu milele ndilo jina lako.

Katika andiko hili MUNGU anaitwa BABA YETU

Yeremia 3:18–19

Siku zile nyumba ya Yuda watakwenda pamoja na nyumba ya Israeli, nao watakuja pamoja, kutoka nchi ya kaskazini, mpaka nchi ile niliyowapa baba zenu iwe urithi wao. Lakini mimi nalisema, Nitawezaje kukuweka pamoja na watoto, na kukupa nchi ipendezayo, urithi ulio mwema wa mataifa? Nami nikasema, Mtaniita, Baba yangu, wala hamtageuka na kuacha kunifuata.

Hapa tunaona MUNGU anataka tumwite Baba kwa sababu yeye ndiye anatupa urithi wa baraka zetu

Malaki 2:10

Je! Sisi sote hatuna Baba mmoja? MUNGU aliyetuumba siye mmoja tu? Basi, mbona kila mmoja wetu anamtenda ndugu yake mambo ya hiana, tukilinajisi agano la baba zetu.

Hapa tunaona kuwa kwa sababu ya uumbaji, sisi ni Watoto wa MUNGU na yeye ni Baba yetu

Mathayo 7:11

Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?

Katika maombi tunayofanya kama wanadamu tunapaswa kutambua sisi ni wana wa MUNGU na MUNGU ni Baba Yetu.

1 Samweli 8:5–7

wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote. Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba BWANA. BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao.

Maandiko yanaonesha Dhahiri kuwa watu wanamkataa MUNGU asiwe mfalme juu yao na kuwatawala. Badala yake walitaka utawala wa wanadamu ili kujiongoza wenyewe.

TUANGALIE KUHUSU MWANA

Katika Ukombozi, MUNGU anasimama kama Mwana

Isaya 9:6–7

Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, MUNGU mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo.

Hapa tunaona mwana mwenye sifa zote za MUNGU kabisa. Kwa hiyo katika ukombozi MUNGU hujifunua kama mwana ambaye ni YESU KRISTO

Katika Utawala, MUNGU Hujifunua kama Bwana

Katika maandiko BWANA ni YESU KRISTO.

Isaya 6:1–3

Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona BWANA ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.

Hapa tunaona nabii isaya anamwona BWANA katika kiti chake cha enzi kama mtawala

Isaya 8:13–14

BWANA wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu. Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu.

Waefeso 2:20–21

Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye KRISTO YESU mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika BWANA

Hapa andiko linaonesha YESU KRISTO ndiye BWANA.

1 Timotheo 6:14–16

kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake BWANA wetu YESU KRISTO; ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, BWANA wa mabwana; ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina.

Yohana 8:58

YESU akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.

Warumi 9:4–5

ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya MUNGU, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka KRISTO kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, MUNGU, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.

Warumi 14:10–12

Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha MUNGU. Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena BWANA, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri MUNGU. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za MUNGU.

Wafilipi 2:10–11

ili kwa jina la YESU kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa MUNGU Baba.

1 Wakorinto 10:9

Wala tusimjaribu BWANA, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka.

Wafilipi 2:5–8

Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya KRISTO YESU; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya MUNGU, naye hakuona kule kuwa sawa na MUNGU kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.

1 Timotheo 3:16

Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. MUNGU alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.

Ufunuo 1:8–18

Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema BWANA MUNGU, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi. Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya YESU KRISTO, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la MUNGU, na ushuhuda wa YESU. Nalikuwa katika ROHO, siku ya BWANA; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu, ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia. Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu; na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini. Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama mwali wa moto; na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kana kwamba imesafishwa katika tanuru; na sauti yake kama sauti ya maji mengi. Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking'aa kwa nguvu zake. Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.

TUANGALIE KUHUSU ROHO MTAKATIFU

Katika Utendaji au Uumbaji MUNGU Ujifunua kama ROHO MTAKATIFU

Ayubu 33:4

ROHO wa MUNGU ameniumba, na pumzi ya Mwenyezi hunipa uhai.

Hapa ROHO MTAKATIFU anatajwa katika eneo la uumbaji. Tuangalie katika utendaji wa karama, huduma katika kanisa

1 Wakorinto 12:4–12

Basi pana tofauti za karama; bali ROHO ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na BWANA ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule; mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na KRISTO.

Maandiko yanasema kazi zote hizi huzifanya ROHO MTAKATIFU

ROHO MTAKATIFU NI MUNGU

Matendo 5:3–4

Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo ROHO MTAKATIFU, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali MUNGU.

Hapa petro anamtambulisha na kumwelezea ROHO MTAKATIFU kuwa ni MUNGU mwenyewe.

Warumi 8:9–10

Lakini ikiwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO wa KRISTO, huyo si wake. Na KRISTO akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki.

Katika andiko hili tunaona kuwa ROHO MTAKATIFU anatajwa kama ROHO wa KRISTO na ROHO Wa MUNGU.

Kwa hiyo BABA, MWANA, ROHO MTAKATIFU huwa ni ofisi au nafasi ambazo MUNGU huwa anatumia kujifunua kwa wanadamu. Hivi ni vyeo vya MUNGU kwa wanadamu na hatupaswi kubatiza kwa vyeo au nafasi za MUNGU.

II: Jinsi Mitume Walivyobatiza Ubatizo wa Jina la YESU

Maandiko yanaeleza wazi kuwa kanisa limejengwa katika misingi ya mitume na manabii. Manabii na mitume wa biblia wanatuma mwongozo sahihi wa jinsi ya kutumika mbele za MUNGU.

Imeandikwa

Matendo 2:20–22

Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye KRISTO YESU mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika BWANA. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya MUNGU katika ROHO.

Tunapaswa kuwafuata mitume kama kielelezo sahihi cha jinsi ya kubatiza watu kwa sababu:

1. Mitume Walielewa kwa Ufunuo Jina Halisi la Wokovu

YESU KRISTO alisema:

Mathayo 28:19

Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;

Lakini mitume walibatiza kwa jina la YESU kwa sababu:

  1. Walitambua kwamba "jina" ni moja (umoja), si majina matatu
  2. Jina hilo lililofunuliwa ni YESU KRISTO
Matendo 4:12

Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo

2. Mitume Walifanya kwa Vitendo (Mfano Halisi)

Kila mahali walipobatiza, walitumia jina la YESU:

Matendo 2:38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha ROHO MTAKATIFU

Matendo 8:16 kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake BWANA YESU. (Walibatizwa kwa jina la YESU)

Matendo 10:48 Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake YESU KRISTO. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha. (Kornelio na nyumba yake)

Matendo 19:5 Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la BWANA YESU. (Wanafunzi wa Efeso)

Hakuna mahali mitume walibatiza kwa maneno mengine tofauti.

3. Waliongozwa na ROHO MTAKATIFU, Si Akili Zao

Mitume hawakukosea, kwa sababu: Walijazwa ROHO MTAKATIFU

Matendo 2:1–4

Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa ROHO MTAKATIFU, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama ROHO alivyowajalia kutamka.

Yohana 16:13

Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

Hivyo walichofanya si bahati mbaya, bali ni mapenzi ya MUNGU yaliyofunuliwa.

4. Jina la YESU Lina Mamlaka Yote

Biblia inasema:

Wafilipi 2:10

ili kwa jina la YESU kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;

Hivyo ubatizo kwa jina la YESU, Unabeba mamlaka kamili, Unahusisha wokovu moja kwa moja

5. Mitume Ndio Msingi wa Mafundisho Sahihi

Matendo 2:42

Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.

Hivyo

  1. Tukifuata wao, tunafuata ukweli
  2. Tukiacha wao, tunaingia katika mapokeo ya wanadamu

Mitume Walivoamuru na Kutenda Kuhusu Ubatizo wa Jina la YESU

1. Mtume Paulo Aliwaagiza Wakristo wa Kolosai

Mtume paulo aliwaagiza wakristo wa kolosai kuwa kila wafanyalo kwa tendo au neno wafanye kwa jina la YESU. Imeandikwa

Wakolosai 3:17

NA KILA MFANYALO, KWA NENO AU KWA TENDO, FANYENI YOTE KATIKA JINA LA BWANA YESU, MKIMSHUKURU MUNGU BABA KWA YEYE.

Ubatizo ni tendo linapaswa lifanyike katika jina la YESU.

2. Mtume Petro Aliagiza Watu Wabatizwe Katika Jina la YESU KRISTO

Matendo 2:38

mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha ROHO MTAKATIFU.

Hapa watu walibatizwa kwa jina la YESU KRISTO na sio nafasi au vyeo vya MUNGU kwa wanadamu anapojifunua kwako.

3. Mtume Petro Aliamuru Akida Kornelio Abatizwe kwa Jina YESU

Matendo 10:48

Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha.

4. Mtume Filipo Aliwabatiza Watu kwa Jina la YESU KRISTO

Imeandikwa

Matendo 8:12–16

12 Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa MUNGU, na jina lake YESU KRISTO, wakabatizwa, wanaume na wanawake.

13 Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka.

14 Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la MUNGU, wakawapelekea Petro na Yohana;

15 ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee ROHO MTAKATIFU;

16 kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake BWANA YESU.

5. Towashi Alibatizwa Katika Jina la YESU KRISTO na Mtume Filipo

Imeandikwa

Matendo 8:36–39

36 Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?

37 Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba YESU KRISTO ndiye Mwana wa MUNGU.

38 Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza.

39 Kisha, walipopanda kutoka majini, ROHO wa BWANA akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.

Kabla ya ubatizo, towashi alipewa msingi wa kuliamini jina la YESU KRISTO na akabatizwa jina hilo la BWANA YESU

Mwisho, mtu anapaswa kubatizwa kwa jina la YESU KRISTO na sio Vyeo au ofisi za MUNGU yaani Baba, mwana na ROHO MTAKATIFU.

6. Mtume Petro Anasema Hakuna Wokovu Nje ya Jina la YESU

Matendo 4:10–12

10 jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la YESU KRISTO wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na MUNGU akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu.

11 Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni.

12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.

Hapa tunaona maandiko yanasema; bila jina la YESU KRISTO hakuna wokovu kwa mwanadamu yeyote chini ya mbingu.

Ubatizo si Desturi tu

Ni muhimu kukumbuka kwamba ubatizo si desturi tu, bali ni agano takatifu kati ya mtu na MUNGU. Biblia inatuonyesha wazi kupitia mitume kwamba ubatizo wa kweli ulifanyika kwa jina la YESU KRISTO na kwa kuzamishwa majini, baada ya mtu kutubu na kuamini.

Kama Ulibatizwa:

  1. Kwa kunyunyiziwa maji,
  2. Au bila ufahamu wa toba na imani binafsi,
  3. Au bila kutumia jina la YESU KRISTO,

basi ni wakati wa kutafakari upya na kuchukua hatua sahihi ya imani.

Matendo 2:38

Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha ROHO MTAKATIFU.

Hii inaonyesha wazi kuwa ubatizo wa kweli:

Unaanza na toba

Unafanyika kwa jina la YESU KRISTO.

Unahusishwa na msamaha wa dhambi

Hata katika Matendo 19:1–5, wale waliokuwa wamebatizwa awali walipofundishwa ukweli, walibatizwa tena kwa jina la YESU KRISTO.

Matendo 19:1–5

Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea ROHO MTAKATIFU mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna ROHO MTAKATIFU hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, YESU. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la BWANA YESU.

Hivyo basi, kama bado hujabatizwa kwa njia hii ya kibiblia, au ulibatizwa kwa kunyunyizwa, usiogope kuchukua hatua ya Imani.

MUNGU anakuita leo:

Njoo kwa toba ya kweli,

Pokea ubatizo sahihi,

Na anza maisha mapya ndani ya KRISTO.

Usikawie; wokovu ni sasa

By

Pastor Obed Joseph Katunzi

Wednesday, March 18, 2026

UDANGANYIFU KWA WATEULE

Udanganyifu - Pastor Obed Katunzi Udanganyifu - Pastor Obed Katunzi
+ + +

Udanganyifu

Udanganyifu ni kitendo cha makusudi cha kusema uongo, kupotosha, au kuficha ukweli ili kumfanya mtu mwingine aamini jambo lisilo la kweli, mara nyingi kwa faida binafsi, kujilinda au kusababisha madhara. Ni kitendo kinachokiuka, kinachohusisha hila, ushawishi wa taarifa za uongo.

Mambo Muhimu Kuhusu Udanganyifu

Kusudi: Hufanywa kwa makusudi ili kufanikisha lengo fulani kama kupata pesa au kumdhuru mtu kwa kumpoteza. Udanganyifu hufanyika kwa njia za injili za uongo ili Mkristo apotee kwenye ramani ya mbinguni.

Aina: Inaweza kuwa ya maneno ya uongo, vitendo (kuficha taarifa) au kupotosha.

Shetani ni baba wa uongo hulipinga Neno la MUNGU sana, kwa sababu Neno la MUNGU ni kweli; maana yeye yupo kinyume cha kweli.

Kwa ufupi udanganyifu ni hila yeyote inayolenga kupotosha ukweli kwa namna hizi mbili:

1Kugeuza Ukweli Kuwa Uongo

Shetani ameweka uongo kwenye imani; baadhi ya imani ni uongo, hakuna ukweli ndani yake. Kuna baadhi ya vitu shetani husema ukweli lakini wenye uongo ndani yake, lakini kuna wakati mwingine husema uongo wote. Kusudi la shetani bado ni lilelile, kumeza watu wengi na juhudi yake ni wote waende kuzimu.

Zaburi 52:2-4

[2]Ulimi wako watunga madhara, Kama wembe mkali, Ewe mwenye hila.

[3]Umependa mabaya kuliko mema, Na uongo kuliko kusema kweli.

[4]Umependa maneno yote ya kupoteza watu, Ewe ulimi wenye hila.

2Kuchanganya Ukweli Pamoja na Uongo

Shetani anajua kabisa kwamba MUNGU hachangamani na uovu, anataka ukweli mtupu katika kanisa; kanisa haliwezi kuwa na uongo ndani yake na MUNGU akawepo, ataondoka tu. MUNGU anataka tujue na kuishika kweli yote.

Wagalatia 5:7-9

[7]Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli?

[8]Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi.

[9]Chachu kidogo huchachua donge zima.

Wateule

Wateule ni watu maalum, waliotengwa kwaajili ya kwenda mbinguni. Yaani ni kwamba watu wengi wanaookoka baada ya kumuamini YESU, lakini wanaokidhi vigezo vya utakatifu ambavyo MUNGU ameweka ni wachache sana; hao ndio huitwa wateule. Maana halisi ya mteule ni mtu aliyeteuliwa, yaani anachaguliwa ndani ya waliochaguliwa kufaa kuliko wale wote.

Mathayo 22:14

[14]Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.

Ni uchambuzi; yaani unachambua kitu mara moja, mara mbili, mara tatu hata mara kadhaa mpaka pale umepata kiwango kizuri halisi unachotaka, kusiwepo na uchafu wowote juu ya hicho kitu. Hivi ndivyo MUNGU anavyofanya juu ya watu wote waliookoka; wateule ni watu ambao wamefikia kiwango anachotaka MUNGU. Shetani anawatafuta sana watu hawa; MUNGU anavyowaandaa, yeye anatafuta kuwapoteza.

Waefeso 4:12-13

[12]Kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;

[13]Hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.

Wakristo ni wengi sana; kila aliyeitwa kwenye neema ya MUNGU kwa njia ya YESU KRISTO, huyo ni Mkristo. Kila Mkristo ni mfuasi wa YESU KRISTO; mtu huyu ameamua kumfuata YESU.

Yohana 1:1-3

[1]Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa MUNGU, naye Neno alikuwa MUNGU.

[2]Huyo mwanzo alikuwako kwa MUNGU.

[3]Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.

Kila kitu chema kinachofanyika hapa duniani kimebebwa na nguvu ya Neno la MUNGU; ndiyo maana shetani anafanya kila mbinu kulipiga vita Neno la MUNGU. Hakuna kilichofanyika pasipo kwa nguvu za MUNGU katika Neno lake. Biblia nyingi siku hizi hazipo salama; shetani ameharibu maana kamili ya mambo ndani ya Biblia, na amenyofoa jumbe kadhaa zenye kuokoa watu wasiishi katika kweli.

Tahadhari

Mmiliki halisi aliyepewa hati miliki ya Biblia (Papa, kiongozi wa Katoliki) ndiye aliyepewa mamlaka na ulimwengu kwa nyakati hizi za mwisho, amehariri na kuondoa vitu muhimu ndani ya Biblia. Anasema yamepitwa na wakati, sheria ni ngumu hazipaswi kufuatwa. Leo hii nakushauri ununue Biblia na uitunze; kuna wakati ambao itakuwa ni vigumu sana kupata Biblia halisi yenye maana kamili MUNGU anayotaka.

Tito 3:3-4

[3]Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana.

[4]Lakini wema wake Mwokozi wetu MUNGU, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa.

Neno la MUNGU ni kweli; asiye na Neno la MUNGU na hamuamini YESU KRISTO, mtu huyo hana akili. Maisha ya kale yaani zamani tulikuwa hatuna akili kwa yale tuliyoyatenda; maana tulifanya ujinga na kuishi kama wajinga kwa sababu hatukuwa na Neno la MUNGU. Lakini sasa tuna akili maana BWANA YESU ametuokoa na kutupa akili.

Matendo ya Mitume 17:30

Basi, zamani zile za ujinga MUNGU alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu.

Shetani anajua umuhimu wa Neno la MUNGU kwa sababu linatupa kuwa na akili; ndiyo maana haachi kulipiga vita ili lionekane halifai. Linda na utunze sana Biblia yako maana kuna hatari ya kupotea baadaye.

+ + +

Biblia za Udanganyifu

1Biblia za Tafsiri Mpya

MUNGU ameagiza maana ya maandiko ibaki yeye alivyokusudia, lakini badala yake kuna Biblia zinaitwa zenye tafsiri rahisi; tafsiri za Kiswahili cha kisasa, wakiwa na dhumuni la kusema Biblia ya zamani ni ngumu. Je ndivyo ilivyo?! Jibu ni hapana. Biblia inapaswa kutafsiriwa kama ilivyo kwa utulivu wa akili na uongozi wa ROHO MTAKATIFU. Kabla ya kusoma Biblia lazima maombi kwanza, mazingira ya utulivu na utulivu wa akili ili ROHO wa MUNGU akupe kuelewa.

Huku ni kutegemea akili zako kumuelewa MUNGU; jambo ambalo haliwezekani. Biblia za Tafsiri mpya hazijaandika jina YESU kuwa ni jina la MUNGU na majina mengine ya MUNGU hayajaandikwa; bali jina la MUNGU ni YEHOVA tu. Biblia hii iliandikwa na kufanywa hivyo na Mashahidi wa Jehova. Maana yake ni kupinga kwamba YESU KRISTO sio MUNGU; je huu sio uongo? Ni uongo mtupu.

2Biblia Zenye Kuzidi Idadi ya Vitabu

Ukristo ni dini ya MUNGU ambayo maana kamili ni wafuasi wa YESU KRISTO. Dini hii inaongozwa na kitabu cha MUNGU yaani Biblia; kila kanisa na kila Mkristo imempasa kufuata Biblia kikamilifu.

Mithali 30:5-6

[5]Kila neno la MUNGU limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio.

[6]Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.

Kwa nini Biblia iwe na vitabu 66 na nyingine iwe na vitabu 72 na wote ni Wakristo?! Biblia sahihi ina vitabu 66. Neno la MUNGU ni hakika na amini; halipaswi kuongezwa wala kupunguzwa na mtu. MUNGU amekataza kwa ukali, laana, na kuzidishiwa mapigo kwa mtu yeyote atakayeongezea Neno la MUNGU.

Mathayo 5:37

[37]Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; Kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.

Kwa Nini Uongeze?

Jambo lolote likizidi katika kiwango au kipimo chake, huwa uongo na udanganyifu; hubeba upotoshaji na hila za kuharibu maisha ya watu kiroho na kimwili. Neno la MUNGU limehakikishwa; hakuna haja ya kuongeza vitu vingine. Ukiongeza maana yake halitoshi; je wewe umemzidi MUNGU maarifa? Jibu ni hapana; kwa hiyo wewe ni mwongo.

Ufunuo wa Yohana 22:18-19

[18]Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, MUNGU atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.

[19]Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, MUNGU atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.

3Biblia za Kisasa (Uongo)

Biblia nyingi siku hizi zimekuja na alama za kishetani na uongo ndani yake. Watumishi wengine wanajua wengine hawajui; halafu ndio wanazitumia kuhubiria madhabahuni. Kwa hali hii watu wengi wanaopotea kwa sababu hawapati maarifa sahihi; wanapata udanganyifu kwa sababu ya Biblia za kishetani. Mikakati ya shetani ipo na Biblia za uongo; ewe Mkristo uwe makini sana na Biblia hizi zilizobadilishwa, ama zilizoongezewa lugha za kisasa.

+ + +

Watu Wanavyodanganywa na Shetani

1 Timotheo 4:1-2

[1]Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;

[2]Kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe.

ROHO MTAKATIFU ananena ndani ya Mtume Paulo, kufunua yatakayotokea. Watu kujitenga wao wenyewe na MUNGU kwa kusikiliza roho za shetani. Hauwezi kufanikiwa katika MUNGU pasipo kuifuata imani ya MUNGU. Kwa sababu walio ndani ya imani wanakuwa ndani ya mapenzi ya ile imani. Jambo la kukutenga na MUNGU ni jambo la hatari sana; inakupasa uliepuke kwa sababu litaondoa tumaini lako na kukuzuia kumuona MUNGU.

Kujitenga ni maamuzi ya mtu mmoja, wawili au zaidi waliokubaliana kuacha jambo fulani kwa kujiepusha nalo. Nyakati za mwisho ni nyakati ambazo uovu ni mwingi; wengi wanazidi kufanya mambo ya kuchukiza na kuumiza mbele za MUNGU na wanadamu. Kitu kinachoweza kukutenga na imani sio kitu cha kawaida; ni kibaya sana.

ROHO MTAKATIFU aliyasema haya kupitia Mtume Paulo ili kusudi watakatifu wawe makini. Kwa udanganyifu watu wengi wanaiacha imani ya utakatifu na kuwa waovu. Hebu jiulize na kutathmini; unaishi ndani ya imani au tayari umeshajitenga? Maana kipindi hiki ni nyakati za mwisho zinazosemwa katika maandiko matakatifu. Kwa sababu muda wowote BWANA YESU anaweza kurudi kuchukua watu wake, yaani sisi tunaomwamini.

+ + +

Mambo Yanayowatenga Watu na Imani

Kwa nini watu wanajitenga na imani? Jibu ni kusikiliza roho zidanganyazo; roho hizo ni roho za shetani, makao yake ni kuzimu, zinashawishi kutenda dhambi na maovu. Anayeongozwa na roho za shetani hutembea katika mapenzi ya shetani na kuacha kufanya mapenzi ya MUNGU.

Kutoka kwenye imani maana yake ni kutolewa kwenye mapenzi ya MUNGU; yaani mambo yote yanayompendeza MUNGU, mtu anaacha kuyafanya. Mtu huyo hawezi kumuona MUNGU maana yuko nje ya MUNGU; atamwonaje MUNGU?

+ + +

Roho Zidanganyazo

Roho nyingi za shetani zinatenda kazi duniani, lakini kwa Mkristo wa kweli ni lazima ahakikishe kwamba ROHO MTAKATIFU tu ndiye kiongozi wa maisha yake ya kila siku.

Waefeso 2:1-3

[1]Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;

[2]Ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;

[3]Ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.

Maana yake; kuna roho mbalimbali za shetani, zinazotenda kazi ndani ya watu wasiotii maagizo ya MUNGU. Roho hizo ndizo zinazoitwa za udanganyifu ili kuwaweka watu katika maisha ya dhambi, watende mabaya na kupinga wema wa MUNGU maishani mwao. Wanaomuamini YESU KRISTO huongozwa na ROHO MTAKATIFU, yaani Roho wa MUNGU. Lakini watu wasioamini, yaani waliomkataa YESU KRISTO na wale waliomuamini kisha wakamuacha kwa kuikana imani (kuasi) huongozwa na roho mbalimbali za ufalme wa kuzimu.

Mifano ya Roho za Ufalme wa Kuzimu

Roho za uzinzi, roho za uongo, roho za tamaa, roho za mauaji (mauti), roho za hasira na ukatili. Roho hizi hutenda kazi sawasawa na kila dhambi kwa kila roho.

+ + +

Kujitenga na Imani

Mwanadamu anayeishi bila kumuamini BWANA YESU huongozwa na mwili na matendo ya mwili ndiyo huamua maisha yake. Mtu anayejitenga na imani ni yule ambaye moja kwa moja amekataa kuamini MUNGU anachosema. Kujitenga na imani ni kukataa kuambatana au kukataa kuongozwa na Neno la MUNGU.

Warumi 10:16-17

[16]Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu?

[17]Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.

Watu wengi wanaabudu miungu kwa sababu ndani ya dunia hii kuna imani nyingi; ila ya kweli ni moja tu, nayo ni kumuamini YESU KRISTO kama Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Biblia imeonyesha miungu mbalimbali inayoabudiwa; zipo sanamu na wapo watu wanaoabudiwa na wamepewa nafasi ya heshima ambayo alitakiwa akae MUNGU tu. Kuna makanisa ambayo wanadamu wamechukua nafasi ya MUNGU kiwango cha kuabudiwa na kanisa. Watu wanawaogopa na kuwaheshimu wachungaji, maaskofu, mitume na manabii wao kuliko hata MUNGU.

Isaya 42:8

[8]Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.

Yaani Neno la MUNGU liseme hivi, mwanadamu aseme hivi; je utamtii mwanadamu kuliko MUNGU? Yaani kuna watu vile ambavyo imewapasa kunyenyekea kwa MUNGU, wananyenyekea kwa wanadamu. Kuna mitume, manabii na wachungaji wanaoheshimika leo kuliko MUNGU; badala ya wawakataze watu wasifanye hivyo, wao wanakubali kupokea utukufu wa MUNGU kwaajili ya nafsi zao.

Matendo ya Mitume 14:9-15

[9]Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa.

[10]Akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda.

[11]Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu.

[14]Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele,

[15]Wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea MUNGU aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo.

Paulo na mitume walipotukuzwa na wanadamu kiasi cha kuabudiwa kutokana na miujiza MUNGU aliyowapa kufanya, walikataa na kusema hapana; sisi ni wanadamu mpeni utukufu MUNGU. Wajibu wa watumishi wa MUNGU wa kweli; hata kama MUNGU atawatumia viwango vikubwa kiasi gani, bado ni wanadamu tu, hawana sifa ya kuabudiwa kama MUNGU.

Isaya 45:22-23

[22]Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni MUNGU; hapana mwingine.

[23]Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa.

MUNGU AMEAPA; maana yake MUNGU ameagiza na amedhamiria kwa nguvu zake; ni maagizo, aabudiwe peke yake. Anavyosema kila goti litapigwa kwake ni kwamba hakuna kama yeye, wala tusimwabudu miungu mingine. Magoti haya ni kwaajili ya kumpigia MUNGU tu, sio mwanadamu au vitu. Hata kama duniani kuna imani nyingi, lakini kumuabudu MUNGU kwa njia ya YESU KRISTO ndio imani ya kweli.

Lakini ninakusihi kwamba shika Biblia na uyaishi maandiko matakatifu yaliyoandikwa humo, maana hiyo ndio Neno la MUNGU. Kama sio Neno la MUNGU nisingeweza kuwa hapa leo; maana ndani ya Neno la MUNGU kuna nguvu za MUNGU na neema nyingi zinazoendelea kubadili watu na kuwatengenezea njia ya haki na usalama, nikiwemo mimi.

Wakolosai 3:16-17

[16]Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu.

[17]Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye.

Neno la MUNGU ni dira; ukipoteza hili umepotea kabisa njia ya kwenda mbinguni.

Dira ni uelekeo unaokuonyesha wewe uko wapi na unakoenda ili kusudi usipotee.

Warumi 6:22

[22]Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa MUNGU, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele.

Watu wamekuwa watumwa wa watu na sio watumwa wa BWANA YESU. Imani hii ni mbaya na imepotoka yenyewe pamoja na watu wanaoishika. Sisi tunamuamini YESU KRISTO ni watumwa wa BWANA YESU na KRISTO YESU ndiye Bwana wetu yaani kiongozi ambaye akisema kitu sharti tufuate na kutii. Utumwa wa Kristo ni kufuata ya KRISTO na Neno la KRISTO; ukifuata Neno la MUNGU hakuna kudanganywa na kupotezwa na roho za uongo.

UONGO ni kitu hatari, kibaya mno; manabii na mitume wa uongo ni wengi sana. Mimi nimeamua kusema ukweli wote wa injili; zamani nilikuwa huko, nilikuwa miongoni mwa wahubiri wa uongo ndani ya chama cha mitume na manabii. MUNGU alinipa neema ya kutoka huko. Hata kama ni gharama kuusema ukweli, lazima iwe hivyo. Inanipasa kugharamia ukweli kama BWANA YESU KRISTO alivyoagiza ili niingie mbinguni.

+ + +

Kupenda Fedha

Shetani amefanya watu kupenda sana fedha ili wasimuone MUNGU. Hii ni mbinu moja wapo na mtego wa kunasa watu wengi hata wateule wa MUNGU. Maisha yanapokuwa magumu ni namna ambayo MUNGU ameruhusu wakati mwingine kama mapito na kipimo cha imani. Wakristo wengi wameshindwa kuvumilia changamoto ya njaa na umaskini; wamedanganywa na kuiacha imani ya kweli, hawana YESU tena mioyoni mwao.

1 Timotheo 6:8-10

[8]Ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.

[9]Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.

[10]Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.

Udanganyifu ambao Shetani amepandikiza kwa watumishi wa uongo, ambao wengine walikuwa wa kweli ni kupenda fedha; kwa sababu hiyo wameiacha imani. Wanafanya miujiza ya uongo na maigizo kwa msemo halisi mazingaombwe; yaani hakuna ukweli.

+ + +

Miujiza na Ishara

Wateule wengi hawajui miujiza sio msingi wa injili bali kweli ya wokovu katika YESU KRISTO. Kama wanajua basi changamoto zimewafanya wasahau. Kwa njia ya miujiza shetani amewapoteza Wakristo wengi waiache imani na kufuata mafanikio tu.

Kumbukumbu la Torati 13:1-4

[1]Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,

[2]Ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;

[3]Wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa BWANA, MUNGU wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda BWANA, MUNGU wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.

[4]Tembeeni kwa kumfuata BWANA, MUNGU wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.

Watu hawajui kwamba miujiza sio maana kuu ya kuzingatia; miujiza sio ishara kuu ya imani. Yaani kutendeka kwa miujiza sio kigezo cha kusema imani fulani ni sahihi. MUNGU ameweka wazi kwamba tuwe waangalifu kuyatazama sana maagizo ambayo ametupa na kuyafanya. MUNGU alisema hivi kwa sababu shetani naye anaweza kutenda miujiza. MUNGU ni Tajiri wa utukufu; hakumnyanganya shetani uwezo na nguvu wala wale malaika wengine walioasi.

+ + +

Kujua Miujiza ya MUNGU

Miujiza ya MUNGU lazima iwe mikubwa kama ikilinganishwa na ya shetani; hata kama isipokuwa ya kutisha sana lengo kuu ni kuwavuta watu kumuamini YESU KRISTO. Lakini kingine ni kwamba miujiza ya MUNGU haipo katika kuamini vitu viitwavyo vya Upako bali jina la YESU KRISTO, pamoja na badiliko la tabia yaani watu kuacha maisha ya dhambi na kuwa wema.

Hata kipindi kile Musa alipokuwa ameagizwa na MUNGU kuwatoa wana wa Israel utumwani, alipewa matendo ya miujiza kama ishara ya kuaminika kwa Waisraeli na mbele ya Farao. Lakini wachawi nao walifanya miujiza kama namna ya kumjibu Musa kwa nguvu za shetani ili kuzuia kusudi la MUNGU.

Kutoka 7:10-13

[10]Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka.

[11]Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.

[12]Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.

[13]Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama BWANA alivyonena.

Unaweza kujiuliza; kwa nini wachawi na wao walifanya miujiza? Lakini MUNGU hakuzuia fimbo zao zisiwe nyoka kama fimbo ya Haruni. Shetani hufanya miujiza ili kuangusha imani; watu wasimzingatie MUNGU. Kwa kuwa wengi wanapenda miujiza wamedanganywa; wanasahau umuhimu wa Neno la MUNGU, hawalisomi, badala yake wameingia kuamini vitu badala ya MUNGU.

Zamani manabii wa uongo waliuawa baada ya kugundulika kwa sababu ilikuwa jino kwa jino katika agano la kale; watu waliongozwa na Torati. Leo hii manabii wa uongo wanapojulikana kuuawa kwao ni watu kuacha kuwafuatilia kwa sababu tupo rohoni. Manabii wa uongo wanapata nguvu za kuendelea kwa sababu ya idadi kubwa ya watu wanaowapigia. Nabii wa uongo akiendelea kuishi ataleta madhara makubwa kwa kuzidi kupoteza watu. Kwa hiyo kipindi cha Torati waliuawa. Nabii Eliya alimtukuza MUNGU dhidi ya Baali; akawachinja manabii wa uongo wote ambao walisema Baali aabudiwe, kwa sababu agizo lilitolewa na MUNGU wauwawe.

1 Wafalme 18:38-40

[38]Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.

[39]Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye MUNGU, BWANA ndiye MUNGU.

[40]Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko.

+ + +

Kisa cha Nabii wa Uongo Redioni

Wakati mmoja hivi; kuna kituo kimoja cha redio cha masafa ya FM niliwahi kwenda pale kutembelea, ni hapa hapa Tanzania. Nilipofika nilikuta muda wa kipindi; amerusha Nabii mmoja hivi, kila siku huwa ni ratiba yake muda huo kurusha kipindi. Yaani kama vile yuko palepale muda huo anahubiri yaani mubashara redioni; kisha anaombea watu na baadhi ya watu wanashuhudia jinsi wameponywa shida na magonjwa yao mubashara.

Lakini yule Nabii hakuwepo; alikuwa amerekodi mahubiri yake na amewapa flash watu wa redioni; wao wameweka inaongea lakini yeye hayupo. Nikawaambia mbona mnafanya huu utapeli, mbona mnashiriki uovu? Yule Nabii alikuwa anaweka simu yake bize; watu wapige simu kuombewa lakini namba yake ya simu inaonyesha anawasiliana na mtu mwingine, kisha anawaambia watume sadaka. Ni uongo mtupu huu.

Nilipowauliza kwanini watu wa redioni wanakubali hayo, wakasema "manabii hao hulipa pesa nyingi, ni faida kwetu, sisi tunaangalia; hata wewe tunaweza kukufanyia hivyo". Nikakataa; hiyo ni dhambi, ni uongo na utapeli. Nilipowauliza kwanini msiache kupokea pesa za hila na utapeli kama huu, wakasema kuendesha vipindi ni gharama; inatakiwa tupate faida na tuwalipe wafanyakazi wa hapa redioni. Wanafanya hivyo wasijue kuwa na wao wanashirikiana na shetani kufanya kazi ya udanganyifu.

Hukumu

Katika hukumu, manabii wa uongo, wamiliki wa redio zenye kuwatangaza manabii wa uongo, na wasikilizaji wote wamehesabiwa hukumu moja kwa sababu wametenda kazi moja na shetani na kupoteza watu. Kwa sababu kama sio redio watu wasingesikiliza huo uongo wakapotea.

Watu wengi wameingia kwenye udanganyifu bila kujua. Chunguza uone jinsi ambavyo watu wengi wanafuatilia redio na vipindi vingapi katika runinga vinavyorushwa na manabii wa uongo. Wamezama kwenye mafundisho ya uongo wanasikiliza roho zidanganyazo; maana hakuna ukweli katika utapeli, hakuna ukweli wenye uongo ndani yake. Hata kama watumishi hao wanatumia Biblia, utapeli wanaoufanya na miujiza ya uongo sio ukweli tena; ni udanganyifu.

2 Wakorintho 6:14-15

[14]Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?

[15]Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?

+ + +

Manabii Wengi Sio Watumishi wa MUNGU

Ndio maana wameweka viwango vya pesa, tena viwango vikubwa tu; yaani ukitaka huduma kwao manabii na mitume hawa, unalipia kwanza na bila kulipia pesa hizo haupati huduma uliyotaka kutoka kwao. Shetani anatumia sana watumishi wanaojifanya kuwa wa kweli ili kuwafanya watu wengi wapotee hasa wale waliamini.

Mfano wa Bei za Huduma za Uongo

Kumuona Nabii: shilingi 300,000

Kununua maji: shilingi 10,000 kwa chupa moja

Mafuta: shilingi 20,000

Kushikana mkono na Nabii au Mtume: shilingi 70,000

Haya yote yanatokea kwa manabii na mitume wa namna hii; hawamtumikii MUNGU bali wanafanya biashara na uongo ambao shetani amewatuma kupoteza maisha ya watu wanaomwamini YESU KRISTO.

Je, BWANA YESU KRISTO alifanya hivi katika maandiko? Aliagiza nini kifanyike ili kuwahudumia watu kiimani, wanaotaka uponyaji? Tuone maandiko matakatifu:

Mathayo 10:7-8

[7]Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.

[8]Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.

Tunaona kumbe BWANA YESU alisema tufanye maombezi kwa watu wote bure; matajiri au maskini. Akaagiza tusipendelee wala kuangalia pesa, cheo, nafasi au mwonekano wa mtu; bali wote kuwaona kama watu wa MUNGU wanaohitaji msaada.

2 Petro 2:1, 3

[1]Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.

[3]Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.

Tito 1:11

[11]Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu.

Kupata mapato ya aibu ni kupata fedha au mali kwa njia zenye uovu na dhambi. Kazi yoyote ambayo haimpendezi MUNGU haupaswi kufanya ewe mwanadamu. Fahamu kwamba kupata pesa wala mafanikio sio shida; ila ni kwa njia ipi? Ni njia inayowezesha au kurahisisha waovu kuwa waovu zaidi au ni njia ya haki?

+ + +

Ushuhuda Mfupi

Siku moja mama mmoja aliyekuwa muuza baa alikuwa anasali kanisani kwa Nabii mmoja hivi. Kumbe yule Nabii alikuwa na tabia ya kwenda kupata pombe katika baa hiyo ambayo yule mama huwa anauza. Yule Nabii alikuwa anavaa kofia ya kufunika uso ili asijulikane; alafu anapokunywa bia huinamia chini kofia imfunike sura yake.

Siku moja yule mama akawa anadai chenji akainama hivi; kumbe ni yule Nabii. Akaanza ugomvi "nirudishie pesa yangu niliyokupa sadaka". Ilikuwa ni ugomvi mkubwa sana.

Fundisho Kutoka Kwa Kisa Hiki

Ndege wafananao huruka pamoja. Yaani kanisa lenye udanganyifu na kuruhusu uhuru wa maisha; mchungaji hawezi kuwa salama! Mafundisho yasiyoleta mabadiliko ya tabia na mienendo ya watu; mchungaji wa kanisa hilo lazima awe na michanganyo. Wachungaji, maaskofu, mitume na manabii wengine hawajaokoka; hata kama waliokolewa basi waliacha imani na kufuata mambo mengine. Pesa, uzinzi na umaarufu vimewaangusha dhambini bila watu kujua.

+ + +

Manabii wa Uongo Kuingia Madhabahuni

Maombolezo 1:10

[10]Huyo mtesi amenyosha mkono wake juu ya matamaniko yake yote; Maana ameona ya kuwa makafiri wameingia ndani ya patakatifu pake; Ambao kwa habari zao wewe uliamuru wasiingie katika kusanyiko lako.

Shetani ameweka mkono wake juu ya kanisa; anatenda kazi kwa nguvu na bidii, anafanya kila anayotaka kwa sababu mawakala yaani manabii na mitume wake wa uongo wanasimama madhabahuni. MUNGU alikataza tangu agano la kale (kipindi cha Torati) manabii wa uongo wasiingie madhabahuni. Anachokifanya shetani ni kuwapa mafundisho ya uongo ambayo yamelenga kupoteza Wakristo. Anafanya kuliondoa tumaini la Wakristo kwa YESU; waweke tumaini katika vitu.

Kanisa tunamhitaji ROHO MTAKATIFU kila wakati; hasa katika muda huu tuliopo ni hatari sana kwa sababu uongo ni mwingi. Kama ROHO MTAKATIFU alivyoyafunua haya; waongo wote anawajua. Tunahitaji kuongozwa naye ili atufunulie wote wa kweli. Muulize akupe kujua wadanganyifu ulionao katika maisha yako. Pengine ni mchumba wako, rafiki yako, na mtu yeyote yule wa karibu amebeba hila za kukuua. Pata muda uombe na ROHO MTAKATIFU atamfunua kwako.

+ + +

Roho za Udanganyifu Zinavyotenda Kazi

1Kanisa Kuongozwa na Watu na Sio MUNGU

MUNGU ameweka uongozi kama mfumo wa utawala kama ilivyo mbinguni. Mchungaji wa kanisa akitenda wema kama MUNGU alivyoagiza katika Neno lake basi ni MUNGU amesema kupitia huyo kiongozi. Mchungaji, askofu, mtume ndio waangalizi wa kanisa; imewapasa kuongoza kanisa na sio waumini ndio waongoze kanisa. MUNGU hapangiwi na malaika cha kufanya; hivyo waumini nao wasimpangie mchungaji ya kuhubiri; MUNGU aongoze kanisa kwa Neno lake kupitia Mchungaji.

Isaya 30:9-11

[9]Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA;

[10]Wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo;

[11]Tokeni katika njia, geukeni mtoke katika mapito; mkomesheni Mtakatifu wa Israeli mbele yetu.

Watu ndio wanaamua nini kihubiriwe na wanampangia mchungaji cha kuhubiri; kama sivyo hawaji kanisani. Watumishi wengi wanatii washirika wao kwa kuogopa wasipungue kanisani; kwa hiyo wanahubiri mapenzi ya washirika. Lakini hawajui kuna hukumu kuhubiri mapenzi ya watu na kuliacha Neno la MUNGU. Idadi kubwa ya watu muda wa ibada sio ukubwa wa kanisa. Kwa Wakristo kila kitu hupimwa namna MUNGU anavyotaka; kipimo cha MUNGU ni utakatifu yaani ukamilifu wa kufuata Neno lake linavyosema.

2Kanisa Kufanana na Dunia

Kanisa kufanana na dunia ni kanisa kuishi kama dunia na mitindo ya kidunia; hii huitwa chukizo la uharibifu. Chukizo la uharibifu ni mambo yanayozuia mtu mwenye juhudi za utakatifu asifike kiwango; watu wasimuamini YESU KRISTO na injili isihubiriwe sawasawa. Haya yanapofanyika kanisani ni moja kati ya ishara za kurudi kwa BWANA YESU. Katika hili ndipo tunajua sifa mojawapo ya kanisa la kweli ni kutokufuata mifumo na taratibu za kidunia.

Danieli 12:9-11

[9]Akasema, Enenda zako, Danieli; maana maneno haya yamefungwa, na kutiwa muhuri, hata wakati wa mwisho.

[10]Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndio watakaoelewa.

[11]Na tangu wakati ule ambapo sadaka ya kuteketezwa ya daima itaondolewa, na hilo chukizo la uharibifu litakaposimamishwa, itapata siku elfu na mia mbili na tisini.

Ni juhudi zote za shetani kukwaza imani; kuzuia utakatifu usipatikane kwa Wakristo. Jambo chukizo ni kitu kibaya au jambo lenye kuudhi, kukwaza, kuangusha na kuua imani ya utakatifu katika YESU KRISTO. Haya ndiyo yamekuwa ya kawaida katika kanisa la leo; yanafanyika kwa uwazi kabisa na wachungaji wengi wamechukuliana nayo pasipo kufanya namna ya kuyaondoa.

+ + +

MUNGU Huyachukia Mambo Haya

1Dhambi

Dhambi ni kitu au jambo kinyume na maagizo ya MUNGU; ni upagani na udunia; yaani kawaida ambazo watu wa dunia (wasioamini) wanafurahia. Watakatifu ni wacha MUNGU; huchukia dhambi.

Mithali 16:17

Njia kuu ya mwenye haki ni kujitenga na uovu; Yeye ashikaye njia yake huihifadhi nafsi yake.

2Upinga Kristo

Ni jumla ya mafundisho yasiyomtukuza YESU; bali mafanikio, utajirisho, maji, mafuta na upako wa vitu. Mafundisho hayo hayazungumzii kazi ya msalaba ya ukombozi na wokovu kwa mwanadamu. Lakini pia mafundisho ya mpinga Kristo hayazungumzii kabisa ujio wa YESU KRISTO kuchukua kanisa lake bali mambo ya ulimwenguni; mambo yenye kuwapotezea muda watu wadhani kuwa maisha ya duniani yana umuhimu kuliko ya milele mbinguni.

3Mambo ya Duniani

MUNGU anataka tuwe kama yeye kwa tabia na mwenendo; maana kwa sura sisi ni mfano tu, yeye ni mtukufu sana hatufanani naye. Mhubiri anayewafurahisha waovu, asiyebadili tabia za waovu kuwa wema kwa mafundisho anayotoa ni mdunia; hafai, kuna udanganyifu ndani yake. Filamu tamthilia, mpira wa miguu, disko, klabu, fasheni; haya ni mambo ya dunia. Watu wa dunia huyafurahia lakini kwa watakatifu ni machukizo ya imani.

1 Yohana 4:5-6

[5]Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia.

[6]Sisi twatokana na MUNGU. Yeye amjuaye MUNGU atusikia; yeye asiyetokana na MUNGU hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu.

Kwa mfano mhubiri anayesema njoo mtu wa dini yoyote, anafanya maombi ya uponyaji bila mafundisho ya imani, badiliko la mienendo na utakatifu; huyo sio wa MUNGU ni wa dunia; yuko kwenye biashara. Kwa mfano pia mhubiri anayesema kila mtu aende kanisani anavyotaka, kwa mavazi na mitindo yoyote bila badiliko; huyo ni mdunia hafai, ni wakala wa shetani kwa njia ya udanganyifu.

1 Petro 1:15-16

[15]Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;

[16]Kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.

Kuhusu Mahubiri

Maneno laini ya kupoteza huhubiriwa na manabii wa uongo; kusudi lao ni kupoteza watu wa MUNGU wasitembee katika dira ya utakatifu. Kusudi kuu la manabii wa uongo ni kuwafanya watu wajisahau; wasijali juu ya utakatifu na safari ya kwenda mbinguni yaani wawaze tu ya duniani.

Warumi 16:17-18

[17]Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao.

[18]Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu.

Ratiba na mwenendo wa ibada; ibada zinazofanyika kwa mfumo wa kipagani na udunia hazitakiwi. Udanganyifu mwingine wa shetani ni kuingiza mambo ya kidunia na ushetani mpaka kanisani; kwenye ratiba za ibada. Siku hizi nyimbo za kidunia, midundo na uimbaji wa kidunia, unyoaji wa nywele na fasheni za mavazi; hapo MUNGU hawezi kuwepo na kanisa litaelekea kuzimu.

Yakobo 1:27

[27]Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za MUNGU Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.

Mathayo 10:16

Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.

Shetani hapendi ukweli; kwa hiyo anapiga vita sana injili ya kweli.

Ni mapambano ya vita na kujipa moyo katika YESU KRISTO, nikiiamini kuwa nitashinda.

Usidhani kuwa ni rahisi kuhubiri injili ya kweli; ni hatari mno.

By
Pastor Obed Katunzi

Tuesday, March 17, 2026

MADHARA YA KULEGEA

 


Kulegea Katika Majukumu - Pastor Obed Joseph Katunzi

Utangulizi

Kila mwanadamu aliye hai duniani ameumbwa kwa kusudi maalum. MUNGU hakumuumba mtu yeyote kwa bahati mbaya, wala hakuna mtu aliye hapa duniani kwa makosa. Kila mtu anao wajibu aliokabidhiwa na Muumba wake, na majukumu hayo yanaweza kujidhihirisha kwa njia tofauti kulingana na nafasi, wito, au mazingira ya maisha ya mtu huyo.

Majukumu haya yanaweza kuwa:

Ya kifamilia (kama mzazi, mtoto, mume, au mke)

Ya kikazi (kama mfanyakazi, meneja, mkulima, mjasiriamali, n.k.)

Ya huduma ya kiroho (kama mhubiri, mwimbaji, mwinjilisti, mshauri, au muombezi)

Ya kijamii (kama kiongozi wa jamii, msaidizi wa wengine, au raia mwema)

Ni muhimu kufahamu kwamba majukumu haya si kwamba yapo tu, bali ni sehemu ya kusudi la MUNGU juu ya maisha ya mtu. MUNGU alipomuumba mwanadamu katika kitabu cha:

Mwanzo 1:28

"MUNGU akawabarikia, MUNGU akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi."

MUNGU alimpa mwanadamu jukumu la kutawala, kuzaa, kujaza dunia na kuitiisha. Hii inaonyesha kwamba majukumu ni sehemu ya agizo la KIMUNGU tangu mwanzo wa uumbaji.

Maisha ya mtu hayawezi kuwa na maana kamili bila kutambua na kutekeleza majukumu yake. Mafanikio ya mtu kiuchumi, kiroho, kihisia au kijamii yanategemea kwa kiwango kikubwa namna anavyotimiza wajibu wake kwa uaminifu. Hata hatima ya mtu — kile atakachokuwa au kufanikisha mwisho wa maisha yake — imo ndani ya uaminifu wake katika kutekeleza majukumu hayo.

+ + +

Kulegea Katika Majukumu

Hata hivyo, changamoto kubwa inayowakumba wengi ni kulegea katika majukumu yao. Ulegevu ni hali ya kupungua kwa bidii, uzito au uthubutu wa kutekeleza majukumu kama ilivyokusudiwa. Mtu anaweza kuwa anaonekana anafanya jambo, lakini hana moto wa ndani, hana uaminifu, au amepoteza mwelekeo.

Yeremia 6:24

"Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na utungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake."

Katika aya hii, tunaona kwamba ulegevu wa mikono si tu wa kimwili, bali ni matokeo ya hali ya ndani ya kiroho na kiakili. Wanadamu wanapopokea habari za hofu, mashambulizi, au hatari, hali yao ya ndani hubadilika. Moyo unayeyuka, na matokeo yake ni:

Kudhoofika kwa juhudi

Kupungua kwa ari ya kufanya kazi

Kupotea kwa tumaini

Kujitoa katika wajibu

Kuingia katika dhiki ya nafsi na mwili

Hali hii inafananishwa na utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa — hali ya uchungu mkubwa, kutoweza kuendelea mbele wala kurudi nyuma. Maumivu makali ambayo mtu hana budi kuyakabili hadi mwisho. Hii ni picha ya uzito wa madhara ya ulegevu: kwamba mtu anapoacha majukumu yake, ni kama mwanamke aliyekaribia kuzaa lakini hana msaada au nguvu ya kumaliza safari yake ya uchungu.

+ + +

Ulegevu Kama Roho

Zaidi ya kuwa hali ya kawaida, ulegevu ni roho ya kishetani inayotumwa ili kuzuia mafanikio na kuyumbisha watu kutoka katika kusudi la MUNGU. Shetani huingiza roho hii ili:

Mtu apoteze ari ya kufanya kazi

Aishi maisha ya uvivu, kuahirisha, na kujitetea

Aache huduma au wajibu wa kiroho

Asitimize ndoto au wito wake

Ahisi hana maana wala mchango katika jamii

Hili ni jambo la hatari sana. Watu wengi wanashindwa si kwa sababu hawana vipawa au nafasi, bali wameshindwa kupigana dhidi ya roho ya ulegevu iliyoingia ndani yao.

+ + +

Uhusiano wa Ulegevu na Uharibifu

Pale ambapo mtu analegea au kupuuza majukumu yake:

Kazi yake inaharibika

Uaminifu wake unapotea

Wale waliomtegemea wanaumia

Kusudi la MUNGU juu yake linachelewa au kuvurugika

Hii ni sawa na askari aliye mstari wa mbele kwenye vita lakini akaamua kupumzika katikati ya mapigano. Atahatarisha maisha yake na ya wengine. Vivyo hivyo, mtu anapoacha majukumu yake, anaacha "safu ya mapambano", na madhara yake huwa makubwa sana — kiroho, kihisia, kifamilia, na hata kimwili.

Kwa hiyo, kabla hatujaanza kuelezea aina za ulegevu na madhara yake, ni muhimu kila mmoja ajitazame mwenyewe kwa uaminifu:

Je, unajua majukumu yako yote kama mzazi, mfanyakazi, Mkristo au kiongozi?

Je, unayatendea kwa uzito, bidii na heshima inayostahili?

Je, umegundua kwamba kuna sehemu ya maisha yako umeshindwa kusimama imara?

Je, unahisi kuna roho ya uvivu au kukata tamaa inayozuia maendeleo yako?

Ikiwa majibu yako yanakuelekeza kwenye ulegevu, basi somo hili ni kwa ajili yako. Ni muda wa kurudi katika nafasi yako na kusema kama Nehemia:

Nehemia 6:3

"Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka."

MUNGU amekupa kazi kubwa sana — iwe ni katika familia, huduma, kazi au maisha yako binafsi. Usikubali roho ya ulegevu ikukatishe tamaa. Katika somo hili, tutaona sababu, madhara, na jinsi ya kushinda ulegevu katika kila eneo la maisha yako.

+ + +

Maana ya Kulegea Katika Majukumu

Kulegea ni hali ya kupungukiwa na nguvu, bidii, uthubutu na uaminifu katika kutimiza majukumu. Ni hali ya kupoteza moto wa ndani uliomuwezesha mtu kuwa na shauku ya kutimiza kile alichoitwa au kupewa afanye.

Isaya 13:7–8

"Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka. Nao watafadhaika; watashikwa na utungu na maumivu; watakuwa na utungu kama mwanamke aliye karibu na kuzaa."

Hii inatuonyesha kwamba kulegea kunaweza kuwa ni matokeo ya woga, habari za kutisha, mashambulizi ya kiroho au kukosa mtazamo sahihi wa kazi au huduma.

+ + +

Sababu za Ulegevu

1. Taarifa na Habari za Hofu

Yeremia 6:24

"Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na utungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake."

Katika maandiko haya, tunaona kwamba kusikia tu habari kunaweza kumvunja mtu nguvu kabisa. Watu wa Israeli waliposikia habari za adui anayewakaribia, hawakupigana kwanza, wala hawakupigwa — walilegea tu kwa kusikia. Hii inaonyesha kwamba habari au taarifa ni silaha kubwa kiroho.

Taarifa mbaya zinaweza kuathiri:

Mawazo yako — zinaingiza hofu, mashaka na sintofahamu.

Kutokuwa na Imani — kunaondoa tumaini na ujasiri wa ndani.

Mtazamo wako — unakosa kuangalia mambo kwa jicho la MUNGU na kuanza kuona kwa jicho la mwili.

Uamuzi wako — mtu anaweza kuahirisha au kuacha jambo muhimu kwa sababu tu ya taarifa.

Mfano wa Maisha Halisi:

Mfanyakazi anapambiwa na wenzake kazini kuwa "bosi hakupendi", anaweza kuanza kulegea kwenye juhudi zake, hata kama hakika hiyo haipo.

Mhubiri anaposikia watu wakimsema vibaya, anaweza kukata tamaa na kuacha huduma.

Taarifa za uongo au uzushi zinaweza kuwa:

Maneno ya wivu

Majungu na umbeya

Tafsiri mbaya za hali fulani

Uongo wa kishetani unaoenezwa ili kuua bidii ya mtu

Jihadhari sana na taarifa unazopokea, na chunguza vyanzo vyake kabla hujafanya uamuzi au kujiruhusu kuathiriwa kiakili na kiroho.

2. Mioyo Inayoyeyuka kwa Hofu

Isaya 13:7

"Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka."

Mioyo inayoyeyuka ni ishara ya hali ya ndani ya kiroho inayovunjika kutokana na hofu, mashaka, au maumivu. Hofu ni mtego wa kiroho unaozuia watu kutekeleza wajibu wao.

Hofu inaleta nini?

Kutokujiamini — mtu haoni thamani wala uwezo ndani yake.

Uoga wa kushindwa — mtu anahisi atashindwa kabla hajaanza.

Kulalamika — mtu anaanza kulaumu mazingira badala ya kutenda.

Kumbuka: Hofu haibebi ukweli wowote halisi, bali ni uvuli wa uongo unaotengenezwa na shetani ili kukufanya usisonge mbele.

Hesabu 13:32–33

32 Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno.

33 Kisha, huko tuliwaona wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.

Hofu hiyo iliwaingiza katika ulegevu — wakaacha kusonga mbele katika ahadi ya MUNGU. MUNGU aliwakasirikia sana hadi wakapoteza urithi wao.

Hofu ni mbolea ya ulegevu — unapoiruhusu ndani yako, unashindwa hata kuanza kutekeleza wajibu wako.

3. Mashambulizi ya Adui (Shetani)

Nehemia 6:2–3

2 Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Walakini wakakusudia kunifanyia mabaya.

3 Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?

Shetani huwa hatulii — kila anapoona mtu yuko katika mstari wa kutimiza kusudi lake, anaanza kupanga mipango ya kumuondoa kwenye mstari huo. Anatumia njia kama:

Hila za kisiasa au kijamii

Maneno ya kukatisha tamaa

Migogoro ya ghafla

Mapingamizi ya kifamilia au kifedha

Nehemia alikuwa na kazi kubwa ya kujenga ukuta wa Yerusalemu. Lakini adui zake walikusudia kumsimamisha — si kwa vita ya moja kwa moja, bali kwa kutumia mialiko ya nje ya kazi — mbinu ya kuvuruga mwelekeo wake.

Kanuni muhimu: Mtu anapopoteza mtazamo wa kile anachokifanya, au kusudi la MUNGU juu ya maisha yake, atakumbwa na ulegevu. Ukishavurugwa mwelekeo, haichukui muda kuanza kulegea mikono na moyo.

Suluhisho ni kuwa na maono thabiti, maombi ya kufunua hila za adui, na roho ya utambuzi kama Nehemia.

4. Manabii wa Uongo

Nehemia 6:12

"Nikatambua, na tazama, siye MUNGU aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; nao Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri."

Shetani ni mjanja — anajua kwamba si kila mtu anaweza kusikiliza watu wa kawaida, hivyo anatumia watu wa dini, wanaoonekana wa kiroho, wenye "karama", lakini wamepotoka mwelekeo wa MUNGU. Nehemia alifuatwa na mtu aliyeonekana kama nabii, ambaye alimtaka aingie hekaluni kwa hofu ya kuuawa. Lakini Nehemia alitambua rohoni mwake kwamba hilo halikutoka kwa MUNGU.

Hatari ya Manabii wa Uongo:

Hutoa "maono" ya hofu na si ya matumaini.

Wanakuvuruga mwelekeo badala ya kukuimarisha.

Wanakuambia uache kazi, huduma, au nafasi, ilhali MUNGU hajasema hivyo.

Wanakutengenezea hofu na mashaka kwa watu wa karibu — kaka, dada, mama au baba na ndugu wa karibu wanaweza kukutengenezea vita vya mwili kwa kukuambia kuwa hawa ni wachawi, mkaingia kugombana mwilini. Wanaweza kukwambia ni wachawi ili usiweze kuwasaidia, na unaingia katika hofu na kutokuwasaidia — na moja kwa moja unaingia katika dhambi.

1 Timotheo 5:8

"Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini."

Waefeso 6:12

"Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."

Njia ya Kujilinda

Pima roho (1 Yohana 4:1) — "Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani."

Linganisha unabii na Neno la MUNGU.

Omba MUNGU akupe utambuzi wa kiroho.

Mtu asipokuwa makini, anaweza kuacha kabisa kusudi lake kwa sababu tu ya "maono" au "ndoto" zisizotoka kwa MUNGU.

5. Ukosefu wa Maarifa ya Kiroho

Hosea 4:6

"Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa."

Mara nyingi mtu anapoonekana mlegevu au asiyewajibika, si kwa sababu ni mvivu, bali hana maarifa ya kiroho kuhusu ukubwa wa majukumu aliyonayo.

Ukosefu wa maarifa huathiri nini?

Utambulisho wako — mtu hajui yeye ni nani katika Kristo.

Majukumu yako — mtu hajui kwa nini yuko kwenye ndoa, huduma au kazi.

Hatima yako — mtu hajui wapi anaelekea, na hivyo hana sababu ya kujitahidi.

Mfano: Mtu akipewa nafasi ya kuwa kiongozi kanisani lakini hajui umuhimu wa wito huo, atafanya kazi hiyo kwa ulegevu, mazoea, na bila bidii yoyote.

Kujua kusudi la MUNGU juu ya maisha yako kunakuwezesha kupigana kulitimiza.

Sababu hizi tano ni baadhi ya silaha kuu anazotumia shetani kuleta ulegevu:

Habari za hofu — zinavunja moyo.

Mioyo inayoyeyuka — inaua ujasiri wa ndani.

Mashambulizi ya adui — yanapoteza mwelekeo.

Manabii wa uongo — wanapotosha watu kutoka kwenye kusudi.

Ukosefu wa maarifa — unafanya watu wachukulie majukumu kijuu juu.

Mtu anayezielewa na kujikinga dhidi ya hizi sababu ataimarika kiroho, atajua kutunza nafasi yake, na atashinda vita ya ulegevu katika maisha yake.

+ + +

Madhara ya Kulegea Katika Majukumu

1. Dhiki na Machungu

Mikono inapolegea, dhiki huingia.

Yeremia 6:24

"Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na utungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake."

Ulegevu huleta uchungu wa nafsi.

2. Baraka Kufungwa

Yeremia 48:10

"Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu; na alaaniwe auzuiaye upanga wake usimwage damu."

Ulegevu katika kazi ya MUNGU huleta laana badala ya baraka. Mtu anaweza kujikuta anafanya kazi lakini hana matokeo kwa sababu ya mkono mlegevu.

3. Kujitoa kwenye Kusudi la MUNGU

Nehemia alifahamu kwamba alikuwa anafanya kazi kubwa. Kama asingekataa mwito wa Sanbalati, angeacha kazi ya MUNGU isifanyike.

Nehemia 6:3

"Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?"

4. Kupoteza Nguvu za Kiroho

Ulegevu huondoa nguvu za kiroho. Hata sala na maombi huonekana kama mzigo. Mtu hachukui tena muda kusali, kusoma Neno au kufanya kazi ya Bwana kwa bidii.

5. Kupoteza Uongozi wa Kiungu

Msumari uliokazwa ukiwa imara, unaweza kubeba mzigo. Lakini ukilegea, kila kitu kinachoegemea juu yake huanguka.

Isaya 22:25

"Katika siku ile, asema Bwana wa majeshi, ule msumari uliokazwa katika mahali palipo imara utalegea; nao utakatwa na kuanguka chini, na ule mzigo uliokuwa juu yake utakatiliwa mbali; maana Bwana amesema haya."

Hii inamaanisha kwamba mtu anapolegea, hata wale waliomtegemea (familia, huduma, jamii) huathirika.

+ + +

Sehemu Ambazo Roho ya Ulegevu Hushambulia

1. Kazini

Roho ya ulegevu inapomshambulia mtu kazini, huonekana kwa njia mbalimbali:

Kuchelewa kazini mara kwa mara

Kutokamilisha kazi kwa wakati

Kutokuwa na ubunifu au hamasa kazini

Kuwalaumu wengine badala ya kuwajibika

Kufanya kazi kwa mazoea, bila ubora au moyo wa kujitoa

Mtu aliyelegea kazini hawezi kuwa baraka mahali pa kazi. Anapoteza fursa za kupandishwa cheo, kuaminiwa zaidi, au kupata baraka kutoka kwa MUNGU.

Mithali 18:9

"Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharabu."

Hii inaonyesha kwamba ulegevu kazini ni sawa na uharibifu. Ukifanya kazi kwa mkono mlegevu, unaharibu: biashara ya mtu mwingine, kipato chako mwenyewe, na imani ya wengine juu yako.

Hatari: Kupoteza kazi au mteja; kukosa mafanikio ya kiuchumi; kuvuruga ushuhuda kama Mkristo.

Suluhisho

Omba neema ya MUNGU kufanya kazi zako kama kwa Bwana:

"Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu." (Wakolosai 3:23)

Kuwa na ratiba na maadili ya kazi. Jifunze kujiongoza hata pasipo kusimamiwa.

2. Huduma ya MUNGU

Katika huduma, ulegevu huingia kwa njia kama: kuchelewa ibadani au kuacha kabisa kushiriki ibada, kupoteza ari ya kuomba au kusoma Neno, kutotii maagizo ya kiroho au kutokuwa tayari kusaidia, kukosa moyo wa kujitoa kwa kazi ya MUNGU.

Mtu aliyekumbwa na roho ya ulegevu kihuduma hufanya mambo ya MUNGU kwa kulazimishwa au kwa mazoea. Hii ni hatari sana kwa sababu huduma si kazi ya kawaida — ni agizo la MUNGU juu ya maisha yako.

Yeremia 48:10

"Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu; na alaaniwe auzuiaye upanga wake usimwage damu."

Ulegevu katika huduma ni laana, siyo tu uzembe. Mtu akiendelea kulegea katika huduma, anaweza:

Kupoteza upako na nafasi yake

Kuwa sababu ya kuanguka kwa wengine

Kuangamiza kizazi chake kwa kutotimiza kusudi la MUNGU

Dalili za ulegevu kiroho:

Maombi ya haraka haraka au ya kulala

Kujisahau katika huduma kwa visingizio vya kazi au familia

Kukwepa majukumu ya kiroho kama kutoa, kushuhudia, au kufundisha

Suluhisho

Kumbuka ni kwa neema ulivyookolewa — jitie moyo kumtumikia MUNGU.

Omba ROHO MTAKATIFU akupe bidii na ari mpya.

Jitahidi kuwa na ratiba ya maombi, Neno, na ibada.

3. Ndoa na Familia

Katika ndoa, roho ya ulegevu inaathiri kwa njia ya: kutokujali hisia za mwenzi wako, kupunguza mawasiliano ya kihemko au ya kiroho, kupuuzia malezi ya watoto, kutokuwa na juhudi ya kufanya ndoa iwe bora.

Wanandoa wengi wameachana si kwa sababu ya dhambi kubwa, bali kwa sababu ulegevu uliingia polepole. Walianza kwa kupunguza mazungumzo, kisha wakaacha kuomba pamoja, kisha kila mmoja akaanza kuishi kivyake.

1 Petro 3:7

"Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe."

Maisha ya ndoa yanahitaji ufahamu na bidii ya kiroho, kiakili na kihisia.

Madhara ya ulegevu katika ndoa:

Migogoro ya mara kwa mara

Kukosekana kwa amani ya nyumbani

Watoto kulelewa katika mazingira ya migogoro

Kukatisha ndoto na huduma za familia

Suluhisho

Rekebisha mawasiliano — ongea, sikiliza, samehe.

Weka ratiba ya maombi ya pamoja.

Fanya juhudi kulinda na kujenga uhusiano kila siku.

4. Afya

Roho ya ulegevu haishambulii tu mambo ya kiroho au ya kiuchumi — huathiri hata mwili wako. Ulegevu katika afya huonekana kwa:

Kutokula vyakula vya afya

Kutojishughulisha kimwili

Kutokunywa maji ya kutosha

Kupuuzia kupumzika au kulala vizuri

MUNGU anatupenda kiroho na kimwili. Mwili ni hekalu la ROHO MTAKATIFU:

1 Wakorintho 6:19

"Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la ROHO MTAKATIFU aliye ndani yenu, mliyepewa na MUNGU? Wala ninyi si mali yenu wenyewe."

Kuacha kujitunza kiafya ni njia ya kulikaribisha gonjwa na uchovu usio wa lazima.

Madhara ya ulegevu katika afya:

Magonjwa ya moyo, kisukari, uzito kupita kiasi

Kushindwa kuwa na nguvu za kiroho (kwa sababu ya uchovu wa mwili)

Kupoteza muda mwingi hospitalini au kutumia fedha nyingi kwa matibabu

Jinsi ya Kukabiliana

Jishughulishe kimwili angalau dakika 20, hata kwa kufanya mazoezi ya kutembea.

Kula kwa utaratibu na uzingatie lishe bora.

Omba neema ya kuwa na nidhamu ya maisha.

5. Maono Binafsi (Ndoto na Malengo ya Maisha)

Hili ni eneo nyeti sana. Watu wengi wamepata maono kutoka kwa MUNGU kuhusu huduma, biashara, kazi au elimu. Lakini baada ya muda, roho ya ulegevu huingia, na mtu: anaanza kukata tamaa, anaahirisha kila kitu, anaacha kujiendeleza, anapoteza matumaini kabisa.

Mithali 29:18

"Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria."

Ukikosa maono au ukayapuuza, utaishi bila nidhamu, bila juhudi, na mwisho bila matokeo. Roho ya ulegevu ni silaha ya shetani ya kuua maono ya mtu kabla hayajatimia.

Dalili za ulegevu kwenye maono:

Kutokuwa na ratiba au mpango wa maendeleo

Kusubiri "hali iwe sawa" kabla ya kuanza

Kusahau kabisa kile MUNGU alikuonyesha au kukusudia

Shughulikia Hivi

Andika tena maono yako na uyaombe kila siku:

"Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji." (Habakuki 2:2)

Tafuta watu wa kukuunga mkono au kukutia moyo.

Chukua hatua ndogo kila siku kuelekea lengo lako.

Roho ya ulegevu hushambulia kila eneo muhimu la maisha, ili kumvunja mtu nguvu kabla hajafikia kilele cha kusudi lake. Ukiiona sehemu yoyote kati ya hizi tano imeathirika: ujue roho ya ulegevu imeshaanza kufanya kazi, na ni lazima uchukue hatua haraka.

Zaburi 18:34

"Ananifundisha mikono yangu vita, Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba."

MUNGU anakupa nguvu mpya leo ya kuipiga roho ya ulegevu katika kila eneo la maisha yako.

+ + +

Suluhisho Dhidi ya Ulegevu

1. Tambua Nafasi Yako na Kazi Ulioitiwa

Kama Nehemia, tambua kwamba unafanya "kazi kubwa". Ukielewa kwamba unahusika katika mpango wa MUNGU, hutapoteza mwelekeo kwa urahisi.

2. Omba kwa Bidii

Zaburi 77:2

"Siku ya taabu yangu nalimtafuta Bwana; Mkono wangu ulinyoshwa usiku, haukulegea; Nafsi yangu ilikataa kufarijika."

Maombi huimarisha mikono iliyolegea. Lazima ujenge utamaduni wa maombi ya kila siku.

3. Pambana na Roho ya Ulegevu

Roho ya ulegevu ni pepo, na YESU aliifukuza kwa mamlaka.

Marko 7:35

"Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri."

BWANA YESU alitumia mamlaka yake kukata vifungo. Sisi pia tunayo mamlaka.

4. Kata Taarifa Mbaya

Epuka vyanzo vya taarifa zinazolegeza moyo wako. Watu wa uzushi, wenye maneno ya kukatisha tamaa, ni silaha ya adui. Linda moyo wako.

5. Omba kwa Ajili ya Moto Mpya

Moto wa kiroho unapowaka ndani yako, ulegevu haupati nafasi.

Zaburi 77:3

"Nilipotaka kumkumbuka MUNGU nalifadhaika; Nilipotaka kutafakari roho yangu ilizimia."

Usikubali roho ya ulegevu ikukatishe tamaa.

Simama imara. Fanya kazi kubwa uliyoitiwa. Hata nisiweze kushuka.

Mwandishi
Pastor Obed Joseph Katunzi

Ubatizo Sahihi ni Huu

Ubatizo Kibiblia Utangulizi Moja ya somo Muhimu sana kwa mkristo anayetarajia...